Refa Aliyekataa Bao la Aziz Ki Apewa Mechi ya Simba Nyumbani CAF
Mwamuzi Dahane Beida, raia wa Mauritania, aliyesababisha mjadala mkubwa baada ya kukataa bao la Stephane Aziz Ki dhidi ya Mamelodi Sundowns, sasa ametajwa rasmi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa ndiye atakayechezesha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mkondo wa pili kati ya Simba SC na RS Berkane kutoka Morocco. Mchezo huo wa kihistoria umepangwa kufanyika wiki ijayo katika Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka CAF, mechi hiyo ya mkondo wa pili itafuata ile ya awali inayotarajiwa kuchezwa Jumamosi hii mjini Berkane, Morocco, ambapo Pierre Ghislain Atcho kutoka Gabon atakuwa mwamuzi mkuu, akisaidiwa na waamuzi wa pembeni Boris Marlaise Ditsoga (Gabon) na Eric Ayimavo Ayamr Ulrich (Benin). Mwamuzi wa akiba mezani atakuwa Patrice Tanguy Mebiame wa Gabon.
Dahane Beida anajulikana sana kutokana na tukio la tarehe 5 Aprili 2024, alipokataa bao la Stephane Aziz Ki katika dakika ya 58 wakati Yanga SC ilipokutana na Mamelodi Sundowns katika mechi ya pili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mchezo huo uliochezwa nchini Afrika Kusini, shuti la Aziz Ki lilionekana kuvuka mstari wa goli, lakini baada ya kupitia mfumo wa VAR, refa huyo alikataa bao hilo, jambo lililozua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka barani Afrika.
Mchezo huo wa Yanga dhidi ya Sundowns ulimalizika kwa sare ya 0-0, na kutokana na sare ya awali pia jijini Dar es Salaam, timu hizo zilienda moja kwa moja katika mikwaju ya penalti. Yanga ilipoteza kwa jumla ya mikwaju 3-2 na kutolewa katika hatua hiyo.
Historia ya Dahane Beida Katika CAF
Tangu mwaka 2019, Dahane Beida amekuwa akichezesha mechi mbalimbali katika mashindano ya vilabu ya CAF. Rekodi zinaonesha kuwa tayari amechezesha jumla ya mechi 25, ambapo ameonyesha kadi za njano 97, kadi nyekundu 3, na ametoa jumla ya penalti 7.
Kwa upande wa timu za Tanzania, refa huyo tayari amewahi kuchezesha mechi moja ya Simba SC dhidi ya Al Ahly ya Misri, katika mashindano ya African Football League (AFL) iliyomalizika kwa sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Oktoba 20, 2023.
Aidha, amechezesha michezo miwili ya Yanga SC – mchezo wa kwanza ukiwa ni fainali ya mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger Juni 3, 2023 nchini Algeria ambapo Yanga walishinda kwa bao 1-0. Mechi ya pili ndiyo hiyo ya utata dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Mchezo huu dhidi ya RS Berkane ni wa kihistoria kwa klabu ya Simba, kwani ni mara yao ya kwanza kufuzu katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004. Michuano hii iliundwa kwa kuunganisha Kombe la Washindi na Kombe la CAF. Hata hivyo, kabla ya hapo, Simba SC iliwahi kufika fainali ya Kombe la CAF na kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Mapednekezo ya Mhariri:
- Majina ya Waliochaguliwa Kidato cha Tano Geita 2025/2026
- Bologna Yaichapa AC Milan na Kubeba Taji la Copa Italia 2025 Baada ya Ukame wa Miaka 51
- KMC Yafufua Ndoto ya Kusalia Ligi Kuu ya NBC 2025/26
- Baada ya Kushuka Daraja, KenGold Yapanga Kurejea Ligi Kuu kwa Nguvu Zote
- Simba Yatolea Tamko Kuhusu Uwanja wa Marudiano CAF na Kuwataka Mashabiki Utulivu
- Mamelodi Sundowns Bingwa Tena wa Ligi Kuu Afrika Kusini 2024/25
- Beki wa Taifa Stars Haji Mnoga Kubaki Salford City kwa Mwaka Mwingine
Leave a Reply