Al Ahly Yatoka Sare na Inter Miami ya Messi Kombe la Dunia la Vilabu FIFA 2025

Al Ahly Yatoka Sare na Inter Miami ya Messi Kombe la Dunia la Vilabu FIFA

Florida, Marekani. Inter Miami inayoongozwa na Lionel Messi imelazimishwa kutoka sare tasa dhidi ya mabingwa wa Misri, Al Ahly, katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia la Vilabu FIFA 2025 uliopigwa usiku wa kuamkia Jumapili kwenye Uwanja wa Hard Rock, jijini Miami. Messi, ambaye aliiongoza timu yake katika mashambulizi makali kipindi cha pili, alionyesha kiwango kizuri cha kujituma, lakini uzoefu na mbinu zake hazikutosha kuivunja ngome ya Al Ahly ambayo ilikuwa imara mwanzo hadi mwisho.

Al Ahly Watawala Kipindi cha Kwanza, Ustari Aokoa Inter Miami

Katika dakika 45 za mwanzo, Al Ahly walionekana kuimiliki mechi kwa kiwango kikubwa, wakitengeneza nafasi nyingi za wazi za kufunga. Hata hivyo, juhudi zao ziligonga mwamba kwa kipa wa Inter Miami, Oscar Ustari, aliyekuwa katika kiwango cha juu mno.

Mshambuliaji hatari wa Al Ahly, Zizo, alipenya hadi ndani ya eneo la hatari na kuangushwa na Telasco Segovia, na kuipatia timu yake penalti dakika ya 43. Mshambuliaji wa zamani wa Aston Villa, Mahmoud Trezeguet, alisimama kupiga mkwaju huo, lakini Ustari kwa mara nyingine aliokoa kwa ustadi mkubwa, na kuiweka Inter Miami kwenye mchezo.

Kocha wa Inter Miami, Javier Mascherano, alikiri wazi kuwa bila Ustari, timu yake isingekuwa salama kipindi cha kwanza. “Tulibebwa na Ustari. Bila yeye, huenda matokeo yangekuwa tofauti kabisa,” alisema baada ya mechi.

Al Ahly Yatoka Sare na Inter Miami ya Messi Kombe la Dunia la Vilabu FIFA 2025

Messi Aongoza Mashambulizi Makali Kipindi cha Pili

Kipindi cha pili kilileta sura mpya kwa Inter Miami. Wakiongozwa na Lionel Messi, waliongeza kasi na shinikizo langoni mwa Al Ahly. Kwa muda mrefu walimiliki mpira, wakitafuta bao la ushindi kwa kila hali.

Messi alikaribia kufunga kwa mpira wa adhabu uliogonga nyavu za pembeni, na tena mwishoni mwa mchezo, alipiga mpira wa mbali uliopanguliwa kwa vidole na kipa wa Al Ahly, Mohamed El Shenawy, na kugonga mtambaa wa panya. El Shenawy aliokoa pia kona ya mwisho ya mchezo kwa kuzuia kwa ustadi kichwa cha Maximiliano Falcon.

Al Ahly Yatoka Sare na Inter Miami ya Messi Kombe la Dunia la Vilabu FIFA 2025

Al Ahly Wavuna Sare Kwenye Uwanja Uliojaa Mashabiki Wao

Licha ya kuwa uwanja ulikuwa Marekani, mashabiki wa Al Ahly walijitokeza kwa wingi na kuutawala kwa sauti, hali iliyomfanya kocha wao mpya, Jose Riviera, kufananisha mazingira hayo na Cairo.

“Tulikuwa na nafasi nyingi kipindi cha kwanza ambazo zingebadilisha matokeo. Lakini hatukuzitumia,” alisema Riviera. “Tulijikuta tukihangaika kipindi cha pili, lakini bado tuna mambo mazuri ya kujifunza. Natumaini mara nyingine tutawapa mashabiki wetu ushindi.”

Ratiba Inayofuata: Mapambano Yanaendelea

Katika kundi hilo A, mchezo wa pili utafanyika leo usiku wa kuamkia Jumatatu kati ya Palmeiras ya Brazil na Porto ya Ureno. Mechi hizo zitakuwa muhimu kuamua hatima ya kundi hilo.

Inter Miami watakabiliana na Porto kwenye mchezo ujao, huku Al Ahly wakitarajiwa kuvaana na Palmeiras siku ya Alhamisi tarehe 19 Juni, 2025. Michezo mingine ya kusisimua inayotarajiwa kupigwa leo ni pamoja na:

  • Bayern Munich vs Auckland City saa 1:00 usiku
  • PSG vs Atletico Madrid saa 4:00 usiku

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB Almasi Kasongo Asimamishwa Kazi na TFF
  2. Steven Mguto Ajiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
  3. Ratiba ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025
  4. Msimamo wa Makundi ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025
  5. Franco Mastantuono Ajiunga Rasmi na Real Madrid | Habari Kamili
  6. Benchi la Ufundi Kengold Njiapanda, Maandalizi Dhidi ya Simba Yakosa Mwelekeo
  7. Mechi Ya Watani Wa Jadi Yanga VS Simba Yasukumwa Mbele Hadi Juni 25
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo