Singida BS Yaendeleza Ubabe Mbele ya Mashujaa na Kubaki Kinara wa Ligi Kuu
Miguel Angel Gamondi ameiongoza Singida Black Stars kuendeleza mwanzo mzuri kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/26 baada ya kuibuka na ushindi wa pili mfululizo. Wakulima wa Alizeti hao waliichapa Mashujaa FC bao 1-0 katika dimba la KMC Complex jijini Dar es Salaam, na hivyo kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi 6 baada ya mechi mbili pekee. Kwa upande mwingine, Mashujaa maarufu kama Wazee wa Mapigo na Mwendo, wamesalia katika nafasi ya tano wakiwa na pointi nne baada ya michezo mitatu.
Rekodi ya Ubabe wa Singida BS Dhidi ya Mashujaa
Mara tatu mfululizo sasa, kila wanapokutana, Singida Black Stars imeonyesha ubabe dhidi ya Mashujaa bila kuruhusu bao. Tangu Oktoba 4, 2024 ambapo Mashujaa walipoteza 0-1 nyumbani Kigoma, historia imeendelea kujirudia. Februari 26, 2025 Singida waliwafunga kwa mabao 3-0 mjini Singida, na sasa Septemba 30, 2025 wamerudia ushindi wa bao 1-0 jijini Dar es Salaam.
Rekodi hizi zinaonesha wazi kuwa Mashujaa wamekuwa wakiteswa kila mara wanapokutana na Singida, hali inayoimarisha hadhi ya Singida kama moja ya timu zenye uthabiti mkubwa msimu huu.
Namna Singida Bs Ilivyopata Ushindi
Katika mchezo uliochezwa katika dimba la KMC Complex, Singida Black Stars ilitawala sehemu kubwa ya mchezo. Bao pekee la ushindi lilifungwa dakika ya 45+5 kupitia straika hatari Elvis Rupia, baada ya timu hiyo kushambulia kwa kasi tangu dakika za mwanzo.
Kiungo mkabaji Khalid Aucho alionekana kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha safu ya kati, huku Clatous Chama akichochea mashambulizi yaliyoiweka Mashujaa katika wakati mgumu muda mwingi wa mchezo.
Kwa upande wa Mashujaa, jitihada zao za kuamka zilionekana zaidi kipindi cha pili ambapo mshambuliaji Ismail Mgunda alijaribu kulenga goli kwa shuti kali. Hata hivyo, umakini wa ulinzi wa Singida ulihakikisha bao la Rupia linasalia kuwa tofauti ya matokeo.
Dakika za Mwisho na Mbio za Kukaa Kileleni Mwa Msimamo
Mashujaa walijitahidi kutafuta bao la kusawazisha dakika tatu za nyongeza kabla ya filimbi ya mwisho, lakini safu ya ulinzi ya Singida BS ilibaki imara hadi mwisho. Ushindi huo umeifanya Singida kuendeleza rekodi ya kutoshinda mechi yoyote msimu huu, na zaidi kuonesha dalili za kuwa miongoni mwa wagombea wakuu wa taji.
Kwa upande wa Mashujaa, hii ilikuwa ni mechi yao ya tatu msimu huu baada ya kuanza na sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania na kupata ushindi wa 1-0 mbele ya Mtibwa Sugar, zote wakiwa nyumbani Kigoma.
Singida BS wao wameendelea kutumia KMC Complex kama uwanja wao wa bahati, wakianza msimu kwa kuilaza KMC 1-0 na sasa kuendeleza ubabe kwa ushindi wa pili kwa matokeo hayo hayo ya bao 1-0.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Ligi Kuu Zanzibar PBZ 2025/2026
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
- Viingilio Mechi ya Simba vs Namungo FC 01/10/2025
- Yanga Sc Yalazimishwa Sare Ya 0-0 Na Mbeya City
- Ratiba ya Mechi za Leo 30/09/2025 Ligi Kuu ya NBC
- Ratiba ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF 2025/2026
- Arsenal yapata ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Newcastle United
Leave a Reply