Singida BS Yapata Pointi ya Kwanza Makundi Kombe la Shirikisho CAF

Singida BS Yapata Pointi ya Kwanza Makundi Kombe la Shirikisho CAF

Singida Black Stars imefanikiwa kupata pointi ya kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Matokeo hayo yametokana na bao la penalti lililofungwa dakika za majeruhi na Marouf Tchakei, likifuta bao la awali la wageni lililowekwa wavuni dakika ya 52 na Langelihke Phili.

Kwa matokeo hayo, Singida BS inavuna alama yake ya kwanza katika Kundi C na kuendelea kusalia nafasi ya mwisho, wakati Stellenbosch ikifika pointi nne na kuongoza kundi hilo baada ya mechi mbili. Otoho d’Oyo na CR Belouizdad zinabaki na pointi tatu kila moja.

Singida BS Yapata Pointi ya Kwanza Makundi Kombe la Shirikisho CAF

Tchakei Aokoa, Historia Yaandikwa Zanzibar

Bao la dakika za majeruhi kutoka kwa Tchakei, ambaye aliingia kipindi cha pili, limeipa Singida BS alama muhimu katika safari yake ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya CAFCC. Hatua hiyo inawafanya kuvunja mwiko uliowahi kuiangusha Namungo FC msimu wa 2020/2021, timu iliyoshindwa kupata hata pointi au bao katika mechi sita za makundi ilizocheza.

Katika mazingira hayo, bao hilo la Tchakei limekuwa tukio muhimu kwa Singida ambayo ilizinduka baada ya kufungwa 2-0 kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria. Penalti hiyo ilitokana na winga wa Singida kuchezewa vibaya ndani ya eneo la hatari, na Tchakei akatekeleza majukumu yake kwa utulivu mkubwa.

Singida Yapoteza Nafasi, Yajilaumu

Licha ya kupata matokeo hayo, Singida BS imebaki na masikitiko kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi, hasa katika kipindi cha kwanza. Katika dakika ya 12, mshambuliaji Elvis Rupia alipata nafasi ya wazi baada ya krosi ya Andre Koffi, lakini hakufanikiwa kumalizia vyema. Dakika 23 baadaye, shuti lake jepesi lilimgonga mwenzake Horso Muaku kabla ya kudhibitiwa na kipa wa Stellenbosch.

Clatous Chama pia alipata nafasi muhimu dakika ya 28, lakini kipa wa wageni aliokoa shuti lake kwa ustadi na mabeki kuondoa hatari hiyo. Katika kipindi hicho cha kwanza, Stellenbosch hawakupiga hata shuti lililolenga lango, wakionekana kuzidiwa katika maeneo yote ya uwanja.

Stellenbosch Wabadilika, Wafunga Bao La Kushtukiza

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi tofauti, wageni wakifanya mabadiliko na kuja na mpango mkali zaidi wa kushambulia. Hatimaye dakika ya 52, Phili aliwatoka mabeki wa Singida na kufunga bao rahisi lililowapa uongozi wa muda na kuwashinikiza wenyeji kuongeza nguvu.

Bao hilo liliwafanya vijana wa Miguel Gamondi kuongeza mashambulizi na kufanya mabadiliko kadhaa yaliyowasaidia kurejea kwenye mchezo. Juhudi hizo ndizo zilizozaa penalti ya dakika za mwisho iliyowekwa wavuni na Tchakei na kuipa timu alama ya kwanza msimu huu katika hatua ya makundi.

Msimamo Kundi C – CAF Confederation Cup

  • Stellenbosch (Afrika Kusini) – Pointi 4
  • Otoho d’Oyo (Congo) – Pointi 3
  • CR Belouizdad (Algeria) – Pointi 3
  • Singida BS (Tanzania) – Pointi 1

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Matokeo ya Stade Malien vs Simba leo 30/11/2025
  2. Kikosi cha Simba vs Stade Malien leo 30/11/2025
  3. Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC Leo 30/11/2025
  4. Msimamo Kundi la Simba Klabu Bingwa 2025/2026
  5. Singida BS vs StellenBosch Leo 30/11/2025 Saa Ngapi?
  6. Msimamo Kundi la Yanga Klabu Bingwa 2025/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo