Azam vs Yanga Yaamishiwa Dimba la Chamazi
Baada ya kutangazwa kufungwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Stadium kupisha maboresho yanayolenga maandalizi ya Africa Cup of Nations 2027, mchezo wa dabi ya Dar es Salaam kati ya Azam FC na Young Africans SC umehamishiwa rasmi katika Uwanja wa Azam Complex Stadium.
Hatua hiyo imeondoa sintofahamu iliyokuwepo kwa mashabiki kuhusu mahali ambapo mchezo huo mkubwa wa Tanzania Premier League utachezwa. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na viongozi wa Azam FC, timu hiyo itakuwa mwenyeji wa dabi hiyo itakayochezwa tarehe 15 Machi 2026 katika dimba la Chamazi.
Dabi ya Dar es Salaam kuchezwa Chamazi
Uamuzi wa kuhamisha mchezo huo umetokana na kufungwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya maboresho ya miundombinu kuelekea fainali za AFCON 2027. Hivyo, Azam FC italazimika kutumia uwanja wake wa nyumbani uliopo Chamazi kwa mchezo huo unaotarajiwa kuvuta hisia kubwa kwa mashabiki wa soka nchini.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria, alithibitisha kuwa dabi hiyo itapigwa Azam Complex badala ya Benjamin Mkapa kama ilivyozoeleka kwa michezo mikubwa ya timu hizo.
“Mechi hiyo itachezwa hapa uwanja wa nyumbani na siyo kwa Mkapa kama ilivyozoeleka, hivyo tunawakaribisha sana mashabiki waje kushuhudia mechi kubwa na nzuri,” alisema Zakaria.
Historia ya mechi zao msimu uliopita
Katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, timu hizi mbili zilikutana mara mbili na kila upande kupata ushindi mmoja.
Katika mchezo wa kwanza, Azam FC iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Gibril Sillah. Hata hivyo, katika mchezo wa marudiano, Young Africans SC ilifanikiwa kulipa kisasi kwa ushindi wa mabao 2-1.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Pacome Zouzoua pamoja na Prince Dube, huku bao la Azam likifungwa na Lusajo Mwaikenda.
Msimamo wa ligi kabla ya dabi
Kwa sasa katika msimamo wa Tanzania Premier League, Azam FC inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 11.
Kwa upande mwingine, Young Africans SC inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 katika idadi hiyo hiyo ya michezo. Hivyo, dabi hiyo ya Machi 15 inaweza kuwa na athari kubwa katika mwelekeo wa mbio za ubingwa wa msimu huu.
Ratiba ya mechi kabla ya Azam vs Yanga
Kabla ya kukutana katika dabi hiyo ya Dar es Salaam, kila timu ina ratiba ya michezo mitatu muhimu katika mashindano tofauti.
Tarehe 5 Machi, Yanga itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Singida Black Stars huku Azam ikisafiri kucheza na Tanzania Prisons katika mechi za ligi. Baadaye tarehe 8 Machi, timu zote mbili zitakuwa nyumbani kucheza michezo ya hatua ya 32 bora ya Tanzania FA Cup. Yanga itakutana na Polisi Tanzania wakati Azam ikipambana na Mbeya Kwanza.
Katika michezo ya mwisho kabla ya dabi hiyo, Azam itakuwa ugenini tarehe 11 Machi kucheza dhidi ya Dodoma Jiji FC, huku Yanga ikicheza ugenini tarehe 12 Machi dhidi ya Tanzania Prisons.
Ibenge aeleza malengo ya Azam
Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, aliwahi kueleza malengo ya timu yake katika msimu huu kuwa ni kupambana ili kumaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
“Malengo yetu ya juu ni kuwa katika nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi, lakini ya chini ni kupunguza tofauti ya pointi kati yetu na Simba na Yanga walio juu yetu,” alisema Ibenge.
Aliongeza kuwa Azam FC inalenga kupunguza pengo la pointi kati yao na wapinzani wao wakubwa, tofauti na msimu uliopita ambapo pengo hilo lilikuwa kubwa.
Mapednekezo ya Mhariri:
- Uwanja wa Mkapa Kufungwa Kupisha Maandalizi ya AFCON 2027
- Azam FC Yalazimishwa Sare ya 2-2 na Pamba Jiji Uwanja wa CCM Kirumba
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
- Wafungaji Bora Ligi Kuu ya NBC Tanzania 2025/2026
- Waamuzi wa Mechi ya Yanga vs Simba 01/03/2026
- Yanga vs Simba 01/03/2026 Saa Ngapi?









Leave a Reply