Othmen Najjar Azungumzia Maandalizi ya Singida BS Kabla ya Kuivaa Yanga
Klabu ya Singida Black Stars imethibitisha kuwa kikosi chake kipo tayari kwa mtihani mgumu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, utakaochezwa Alhamisi, Machi 5, 2026. Meneja Mkuu wa klabu hiyo, Othmen Najjar, amesema maandalizi ya timu yamejikita katika kuongeza umakini wa wachezaji, kudumisha nidhamu ya mchezo na kutumia ipasavyo nafasi watakazopata uwanjani.
Najjar alieleza kuwa kikosi kimekuwa kikijiandaa kwa umakini mkubwa kuelekea mchezo huo, huku akisisitiza kuwa wachezaji wanaelewa ubora wa wapinzani wao.
“Sote tunajua ubora wa Yanga, hivyo itakuwa mechi ngumu. Naamini matokeo ya mechi iliyopita yameongeza kitu kwa upande wetu. Ni wazi kwamba itakuwa mechi tofauti kabisa na iliyopita lakini hii ni nafasi kwa wachezaji kuonyesha yale ambayo tumekuwa tukiyafanyia kazi,” alisema.
Meneja huyo pia alikiri kuwa rekodi ya mikutano ya hivi karibuni haiko upande wa Singida Black Stars, akieleza kuwa Yanga imeshinda mechi sita mfululizo dhidi ya timu hiyo katika mashindano yote. Hata hivyo, amesema historia hiyo haitoi presha kwa kikosi chake bali inaongeza hamasa ya kubadilisha matokeo.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana ilikuwa katika Kombe la Mapinduzi 2026, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0 katika hatua ya nusu fainali. Katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara 2024/2025, Singida Black Stars pia ilipoteza mechi zote mbili dhidi ya wapinzani hao, ikifungwa 1-0 nyumbani kabla ya kupoteza tena 2-1 jijini Dar es Salaam.
Najjar amesema Singida Black Stars itaingia uwanjani ikiwa na heshima kwa wapinzani wao lakini bila woga.
“Tunaiheshimu Yanga lakini tutacheza kwa kujiamini na kwa uwezo wetu wote,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa benchi la ufundi limeweka mkazo katika kuimarisha safu ya ulinzi pamoja na kuongeza ushirikiano wa timu kwa ujumla, akisisitiza kuwa umakini katika kutumia nafasi utakuwa muhimu katika mchezo huo.
Kwa sasa Singida Black Stars ina pointi 19 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikishika nafasi ya tisa baada ya mechi 11. Baada ya mchezo dhidi ya Yanga, timu hiyo itakutana na Songea United Machi 8, 2026 katika hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho, kabla ya kurejea tena Ligi Kuu Bara kumenyana na Simba Machi 11, 2026.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Uwanja wa Mkapa Kufungwa Kupisha Maandalizi ya AFCON 2027
- Azam FC Yalazimishwa Sare ya 2-2 na Pamba Jiji Uwanja wa CCM Kirumba
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
- Wafungaji Bora Ligi Kuu ya NBC Tanzania 2025/2026
- Waamuzi wa Mechi ya Yanga vs Simba 01/03/2026
- Yanga vs Simba 01/03/2026 Saa Ngapi?









Leave a Reply