Bingwa Wa Ngao ya Jamii 2024 ni Yanga Sc, Yailaza Azam FC 4-1 Katika Fainali
Klabu ya Yanga SC imeendelea kuthibitisha ubora wake katika soka la Tanzania baada ya kuanza msimu wa 2024/2025 kwa kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii 2024 kwa ushindi wa kishindo wa mabao 4-1 dhidi ya Azam FC. Fainali hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilikuwa ya kusisimua na kuvutia maelfu ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia mpambano huo wa kuvutia.
Mchezo wa fainali ulianza kwa kasi, huku Azam FC wakionekana kutaka kudhibiti mchezo mapema. Jitihada zao zilidhihirika dakika ya 13 ya mchezo walipofanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo wao mahiri, Feisal Salum maarufu kama “Fei Toto”. Bao hili lilikuja baada ya shambulizi la haraka lililowashangaza mabeki wa Yanga SC.
Hata hivyo, furaha ya Azam FC haikudumu muda mrefu, kwani Yanga SC walisawazisha dakika ya 19 kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Prince Dube. Goli hilo liliwapa nguvu zaidi vijana wa Jangwani, ambao walianza kushambulia kwa kasi kubwa. Mashambulizi hayo yalipelekea Yoro Diaby wa Azam FC kujifunga bao akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na beki wa pembeni wa Yanga, Chadrack Boka.
Kipindi cha Kwanza Chamalizika kwa Ushindi wa Yanga
Yanga SC haikuishia hapo, kwani waliongeza bao la tatu kabla ya kwenda mapumziko kupitia kwa kiungo wao mahiri, Stephane Aziz Ki. Licha ya Azam FC kujaribu kurudi mchezoni, Yanga SC walidhibiti mchezo na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-1.
Kipindi cha Pili: Azam FC Yajaribu Kurudi Mchezoni
Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji, wakijaribu kurekebisha makosa ya kipindi cha kwanza. Licha ya juhudi hizo, walishindwa kupata nafasi nyingi za wazi za kufunga, huku Yanga SC wakionekana kudhibiti mchezo kwa umakini mkubwa.
Yanga SC nao walifanya mabadiliko yao, ambapo mabadiliko hayo yaliweza kuzaa matunda baada ya Clement Mzize aliyekuwa ameingia kutoka benchi kufunga bao la nne baada ya pasi safi kutoka kwa Clatous Chama. Goli hilo liliwazima kabisa Azam FC na kuhakikisha ushindi wa Yanga SC unakuwa wa kishindo.
Safari ya Yanga SC Kuelekea Ubingwa
Yanga SC waliingia kwenye fainali hii baada ya ushindi wa goli 1-0 dhidi ya watani zao Simba SC katika hatua ya nusu fainali, huku Azam FC wakiichapa Coastal Union kwa mabao 5-2 ili kufuzu fainali. Mchezo huu wa fainali ulithibitisha kwa mara nyingine ubora wa Yanga SC, ambao wamekuwa wakionesha kiwango cha juu katika mashindano mbalimbali.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo Yanga VS Azam Leo Fainali Ngao ya Jamii 2024
- Kikosi Cha Yanga Vs Azam Fc Fainali Ngao ya Jamii 11/08/2024
- Simba Warudi Sokoni Kusaka Mshambuliaji Mpya Kuongeza Makali
- Tanzania Yamaliza Olimpiki 2024 Mikono Mitupu
- Matokeo ya Simba Vs Coastal union Leo Ngao ya Jamii 11/08/2024
- Ratiba ya Mechi za Yanga Ligi Kuu NBC 2024/2025
- Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/2025 (NBC Premier league)
Weka Komenti