Dembélé Amechaguliwa Kuwa Mchezaji Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya 2024/25
Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain (PSG), Ousmane Dembélé, ameandika historia mpya katika soka la Ulaya baada ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2024/2025. Tuzo hiyo imemjia kufuatia msimu wa kipekee alioonesha akiwa katika safu ya ushambuliaji ya PSG, ambayo imetawala mashindano hayo kwa kiwango cha juu.
Dembélé, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwa na uwezo wa kipekee katika soka la kisasa, aliongoza kikosi cha PSG kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Inter Milan katika fainali iliyofanyika Jumamosi ya Mei 31, 2025, kwenye dimba la Allianz Arena. Ushindi huo ulikuwa ni wa kishindo na wa kihistoria, na mchango wake ukawa wa kuigwa, na hatimaye kumfanya kuwa nyota wa msimu.
Katika safari ya PSG kuelekea taji hilo, Dembélé alicheza mechi 15, akitumia jumla ya dakika 1,163 uwanjani. Katika muda huo, alihusika moja kwa moja na mabao 14, akifunga nane na kutoa pasi sita za mabao. Takwimu hizi si tu zinaonesha ufanisi wake wa kiuchezaji, bali pia uwezo wake wa kubadili matokeo ya mchezo kwa ubunifu na kasi ya hali ya juu.
Kwa mujibu wa timu ya wataalam wa kiufundi ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Dembélé ameonekana kuwa mchezaji aliyesababisha hofu kwa wapinzani kwa mijongeo yake ya kushambulia, huku pia akishuka chini kusaidia safu ya kiungo pale ilipohitajika. Kati ya viwango vilivyopimwa, umbali wa Kilomita 126.11 alioukimbia katika mashindano hayo ni ushahidi wa kujituma kwake na mchango mkubwa alioutoa kwa timu yake.
Katika kikosi cha PSG msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, Dembélé ameibuka kinara wa mabao, hali iliyomuweka mbele ya washambuliaji wenzake na kumpa nafasi ya kipekee kama nembo ya mafanikio ya timu hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dembélé hakuficha furaha yake: “Tangu nikiwa mtoto mdogo nilitamani kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kufika fainali na kushinda ubingwa ni jambo lisiloelezeka kwa maneno. Ninajivunia safari yetu kama timu na mafanikio yangu binafsi. Hii ni ndoto iliyotimia,” alisema kwa hisia.
Tuzo ya mchezaji bora kwa Dembélé inamuweka kwenye orodha ya nyota waliowahi kutwaa tuzo hiyo miaka ya hivi karibuni, akifuata nyayo za Vinicius Junior wa Real Madrid aliyeshinda mwaka 2023/2024, Rodri wa Manchester City aliyeshinda msimu wa 2022/2023 na Karim Benzema aliyekuwa mshindi wa msimu wa 2021/2022.
Kwa upande mwingine, PSG imeendelea kung’ara katika tuzo za msimu huu baada ya mchezaji wao chipukizi, Desire Doue, kutangazwa kuwa Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya 2024/2025. Doue, mwenye umri wa miaka 19, amecheza mechi 16 na kutumia dakika 742 uwanjani, ambapo amehusika na mabao 10 – akifunga matano na kutoa pasi tano za mabao. Kwa mujibu wa takwimu, chipukizi huyo amekimbia jumla ya Kilomita 91.2 katika mashindano hayo, akionesha uwezo mkubwa wa kiufundi na stamina.
Tuzo hiyo inamweka Doue katika orodha ya wachezaji mahiri waliowahi kutwaa tuzo hiyo, akiwafuata Jude Bellingham (2023/2024), Khvicha Kvaratskhelia (2022/2023) na Vinicius Junior (2021/2022).
Kwa kumalizia msimu kwa mafanikio makubwa, wachezaji 11 wamechaguliwa kuunda kikosi bora cha Ligi ya Mabingwa Ulaya 2024/2025. Kipa bora alikuwa Gianluigi Donnarumma (PSG), huku safu ya ulinzi ikiongozwa na Achraf Hakimi, Marquinhos na Nuno Mendes (PSG) pamoja na Alessandro Bastoni wa Inter Milan. Kiungo wa kati aliyechaguliwa ni Vitinha wa PSG akishirikiana na Declan Rice wa Arsenal, huku safu ya ushambuliaji ikijumuisha Desire Doue na Ousmane Dembélé wa PSG pamoja na Lamine Yamal na Raphinha kutoka Barcelona.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Siku ya Kuripoti Chuo cha Polisi Moshi 2025 kwa Vijana Waliochaguliwa
- Wafungaji Bora Klabu Bingwa Afrika CAF 2024/2025
- Fiston Mayele Ndie Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika CAF 2024/2025
- Washindi Tuzo Za Baraza La Michezo Tanzania BMT 2024
- Pyramids Yabeba Ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika 2024/2025 kwa Mara ya Kwanza Kihistoria
- Wachezaji wa Simba Walioitwa Kwenye Kikosi cha Timu ya Taifa June 2025
- Hawa Apa Maofisa wa Mechi ya Nusu Fainali CRDB Bank Federation Cup 2024/2025
- Kikosi cha Taifa Stars kilichoitwa kambini Kuelekea COSAFA na Mechi ya Kirafiki
Leave a Reply