Fadlu Davids Atambulishwa Kama Kocha Mkuu wa Raja Casablanca ya Morocco

Fadlu Davids Atambulishwa Kama Kocha Mkuu wa Raja Casablanca ya Morocco

Klabu ya Raja Casablanca ya nchini Morocco imetangaza rasmi kumteua Bwana Fadlu Davids kuwa Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, hatua inayokuja muda mfupi baada ya kocha huyo kuondoka ndani ya Simba SC ya Tanzania. Davids alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lililoshiriki katika mafanikio ya kihistoria ya Raja msimu wa 2023/24 alipokuwa Kocha Msaidizi, kipindi ambacho timu hiyo ilitwaa ubingwa wa ligi kuu ya Morocco Botola Pro bila kupoteza mchezo wowote na pia kutwaa Kombe la Throne.

Fadlu Davids Atambulishwa Kama Kocha Mkuu wa Raja Casablanca ya Morocco

Uteuzi Rasmi na Maelezo ya Klabu

Kupitia taarifa iliyotolewa Septemba 22, 2025, Raja Casablanca ilithibitisha kuwa Davids anachukua nafasi ya kocha Lassad Chabbi aliyemaliza muda wake. Taarifa ya klabu hiyo ilieleza kuwa uteuzi wa Davids umezingatia uzoefu wake wa awali ndani ya klabu, jambo linaloimarisha mshikamano wa wachezaji na kusaidia kufanikisha malengo ya kimichezo na kitaasisi ya Raja.

Klabu pia ilibainisha kuwa hatua hii ni sehemu ya mwendelezo wa mradi mpya wa maendeleo ya Raja Club Athletic, unaolenga kujenga msingi thabiti wa mafanikio ya muda mrefu. Aidha, ilisisitiza kuwa inategemea uungwaji mkono wa mashabiki wake waaminifu katika kipindi hiki kipya cha mabadiliko.

Safari ya Davids kutoka Simba SC

Fadlu Davids anarejea Morocco baada ya kuitumikia Simba SC kwa siku 444, tangu alipojiunga Julai mwaka 2024.

Taarifa za kuondoka kwake ziliibuka mara tu baada ya kikosi cha Simba kurejea nchini kutoka Botswana kupitia Afrika Kusini, safari ambayo haikuwa na Davids pamoja na wasaidizi wake. Baadaye ilibainika kuwa kocha huyo alikuwa ameondoka kuelekea Morocco kwa ajili ya kukamilisha makubaliano na Raja Casablanca.

Kuthibitisha taarifa hizo, Simba SC ilitoa tamko rasmi la kuagana na Davids, ikieleza kuwa makubaliano ya kusitisha mkataba yalitokana na maombi binafsi ya kocha huyo. Uongozi wa Simba ulimshukuru kwa mchango wake muhimu, ukiwemo kuipeleka timu hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita pamoja na kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Ratiba ya Mechi za Leo 22/09/2025
  2. Matokeo ya Gaborone United vs Simba leo 20/09/2025
  3. Hiki Apa Kikosi cha Simba vs Gaborone United leo 20/09/2025
  4. Viwango Vya FIFA Duniani 2025 (FIFA Rankings)
  5. Taifa Stars Yashuka Nafasi Nne Katika Orodha Mpya ya Viwango vya FIFA
  6. Benfica Yampa Mourinho Kibarua cha Kuiongoza kwa Miaka Miwili
  7. Yanga Yaanza Msimu wa Ligi ya Mabingwa Kwa Ushindi wa 3-0
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo