Fei Toto Atamani Bato Lake na Aziz Ki liendelee
Feisal Salum, maarufu kama Fei Toto, kiungo mshambuliaji wa klabu ya Azam FC, amefunguka kuhusu tamaa yake ya kuendeleza ushindani wake wa karibu na Stephane Aziz Ki. Fei Toto anasema kwamba, licha ya wao kuwa wapinzani katika kinyang’anyiro cha mfungaji bora msimu uliopita, ushindani wao umemsaidia sana kuimarika katika mchezo wake.
Msimu wa 2023/2024 ulikuwa wa ushindani mkali kati ya Fei Toto na Stephane Aziz Ki. Wachezaji hawa walionesha viwango vya juu, wakipambana kwa karibu katika mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora wa ligi. Aziz Ki aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 21, huku Fei Toto akiibuka wa pili na mabao 19, tofauti ya mabao mawili pekee.
Fei Toto alieleza kuwa, licha ya kushindwa kuchukua taji hilo, anaona ushindani wao ulikuwa chachu ya mafanikio yake binafsi. “Mimi sio mshambuliaji halisia, lakini kila ninapopata nafasi ya kufunga, nakuwa na furaha kubwa. Ushindani wangu na Aziz Ki umekuwa msaada mkubwa kwangu, kwani nimejifunza mambo mengi kutoka kwake,” alisema Fei Toto katika mahojiano na Mwanaspoti.
Fei Toto alieleza kuwa, mbali na ushindani wao wa uwanjani, alikuwa akimfuatilia sana Aziz Ki kwa karibu.
Alisema kila wakati alipokuwa akiangalia mechi za Aziz Ki, alihamasishwa zaidi kufanya vizuri. “Nilipokuwa nikiona Aziz Ki anafunga, ilikuwa inanipa hasira ya kujituma zaidi ili nami nifunge,” alisema.
Hii inaonesha jinsi gani ushindani wa kiuanamichezo unavyoweza kuwa na faida kubwa kwa wachezaji binafsi. Fei Toto anasema kuwa, kwa kujifunza kutoka kwa Aziz Ki, amepata uzoefu unaomsaidia kuimarika na kuwa bora zaidi.
Tamaa ya Kuendeleza Ushindani
Kwa sasa, Fei Toto anatamani ushindani huu uendelee msimu huu wa 2024/2025. Anaamini kwamba, kupitia ushindani huo, atazidi kujijenga kama mchezaji na kufikia viwango vya juu zaidi. “Natamani bato lake na Aziz Ki liendelee, kwani linanijenga na kunitoa sehemu moja kwenda nyingine,” alisema Fei Toto.
Malengo ya Msimu Mpya
Fei Toto pia alizungumzia malengo yake binafsi na ya timu yake ya Azam FC kwa msimu huu. Anasema kuwa, licha ya mwanzo mgumu katika mechi za kwanza, Azam FC bado wana nafasi ya kujiimarisha na kupambania mataji. “Msimu uliopita ulikuwa mzuri kwangu binafsi, sasa nataka kuhakikisha naendeleza ubora wangu na kusaidia timu kufikia malengo makubwa,” alisema.
Fei Toto ana ndoto ya kutwaa taji la ligi kuu na kombe la Shirikisho akiwa na Azam FC. Anasema kuwa amewahi kushinda mataji akiwa nje ya Azam FC, lakini sasa anataka kuleta mafanikio hayo akiwa na timu yake ya sasa. “Hakuna kinachoshindikana, nikiwa na Azam FC natamani kuipa timu mataji, na naamini hili linawezekana,” aliongeza.
Ushindani wa Ligi na Changamoto za Msimu Huu
Msimu huu umeanza tofauti sana kama wengi walivyo fikiri kwa Azam FC baada ya kuambulia sare mbili mfululizo katika mechi za mwanzo dhidi ya JKT Tanzania na Pamba FC. Hata hivyo, Fei Toto anaamini kwamba timu yake bado ina nafasi kubwa ya kurejea kwenye ubora wao. “Mpira una matokeo matatu; kushinda, sare au kupoteza. Matokeo mabaya ya michezo ya mwanzo siyo sababu ya kutukatisha tamaa. Tunaendelea kupambana na kujiimarisha,” alisema Fei Toto.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Kenya, Uganda na Tanzania Kuandaa CHAN 2024 – Fainali Kuanza Februari
- Nkata Ataja Sababu 4 za Kagera Sugar Kuanza Ligi Kuu Vibaya
- Mambo Hadharani, Kilichomuondoa Kocha KenGold Chafichuka
- Majina ya Walioitwa Kwenye Usaili Utumishi 2024
- Matokeo Kagera Sugar vs JKT Tanzania Leo September 16 2024
- Viingilio Mechi ya Simba Vs Al Ahli Tripoli 22/09/2024
- Ahmed Ally Athibitisha Usalama wa Kikosi cha Simba Libya
Weka Komenti