Baada ya Kushuka Daraja, KenGold Yapanga Kurejea Ligi Kuu kwa Nguvu Zote

Baada ya Kushuka Daraja, KenGold Yapanga Kurejea Ligi Kuu kwa Nguvu Zote

Mbeya, Tanzania; Pamoja na kushuka daraja baada ya msimu mmoja pekee katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, timu ya KenGold haijakata tamaa. Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Omary Kapilima, amesema wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanajenga upya kikosi chao kwa lengo la kurejea kwa kasi katika ligi kuu msimu ujao kupitia Ligi ya Championship.

KenGold ilishuka daraja baada ya kushindwa kufikia viwango vya ushindani msimu wa 2024/2025 wa Ligi Kuu, ambapo timu hiyo ilikusanya pointi 16 kati ya michezo 28. Katika rekodi hiyo, walishinda michezo mitatu pekee, wakatoka sare mara saba na kupoteza michezo 18. Timu hiyo ilifunga jumla ya mabao 22 na kuruhusu mabao 52—ikiwa ni idadi ya pili kwa kufungwa zaidi baada ya Fountain Gate.

Baada ya Kushuka Daraja, KenGold Yapanga Kurejea Ligi Kuu kwa Nguvu Zote

Mikakati ya Kurudi Ligi Kuu Msimu Ujao

Kocha Kapilima amesema kuwa iwapo ataendelea kuwa sehemu ya benchi la ufundi msimu ujao, hatua ya kwanza itakuwa ni kukutana na uongozi wa timu kujadiliana namna ya kuwashawishi wachezaji waliocheza vizuri kubaki kikosini.

Wachezaji hao ni pamoja na waliotua katika dirisha dogo la usajili kama Benard Morrison, Seleman Rashid ‘Bwenzi’, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani, Zawadi Mauya, Sadala Lipangile na Kyala Lasa.

“Kwa kuwa tunazo mechi mbili zilizobaki, ni mapema kusema kama nitaendelea kuwa sehemu ya timu au la, lakini endapo nitabaki, nitajadiliana na uongozi kuhakikisha nyota waliotoa mchango mkubwa hawahama, ili tuwe na kikosi imara kwa ajili ya Championship,” alisema Kapilima.

Changamoto na Tathmini

Kapilima, ambaye ni beki wa zamani wa Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alifafanua kuwa moja ya sababu kubwa za kushuka daraja ilikuwa ni udhaifu katika safu ya ulinzi. Alisema karibu kila mchezo waliucheza, waliruhusu bao, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa matokeo mabaya.

Ameeleza kuwa kwa sasa timu imekubali matokeo na inalenga kutumia mechi mbili zilizobaki kuhitimisha msimu kwa heshima na kujiandaa mapema kwa mashindano ya Championship msimu ujao.

“Tunakubali hali tuliyonayo sasa. Lengo letu ni kutumia mechi hizi mbili kama sehemu ya kuimarisha morali ya wachezaji na kuweka msingi wa maandalizi ya msimu ujao. Tathmini kamili ya kikosi itafanyika mara baada ya ligi kumalizika,” aliongeza Kapilima.

Katika hatua ya kujiandaa na msimu ujao, uongozi wa KenGold unakabiliwa na changamoto ya kusimamia mabadiliko makubwa ya kikosi, kwani mikataba ya wachezaji wengi inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Hii ni hali inayohitaji usimamizi makini ili kuepuka kuondokewa na wachezaji muhimu ambao wanaweza kusaidia timu kurejea Ligi Kuu kwa mafanikio.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Simba Yatolea Tamko Kuhusu Uwanja wa Marudiano CAF na Kuwataka Mashabiki Utulivu
  2. Mamelodi Sundowns Bingwa Tena wa Ligi Kuu Afrika Kusini 2024/25
  3. Beki wa Taifa Stars Haji Mnoga Kubaki Salford City kwa Mwaka Mwingine
  4. Fountain Gate Njia Panda Baada ya Kichapo Dhidi ya JKT
  5. Timu Zilizoshuka Daraja Ligi Kuu ya NBC 2024/2025
  6. Matokeo ya Yanga Vs Namungo FC Leo 13/05/2025
  7. Dickson Ambundo Ajiweka Sokoni Huku Fountain Gate Ikipambana Kubaki Ligi Kuu
  8. Yanga Yaanza Kutega Mitego ya Kumnasa Marcel Koller, Aliyekuwa Kocha Ahly
  9. Simba Yaendelea Kugawa Dozi Kwa Kila Anayekutana Naye Ligi Kuu
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo