Kikosi cha Simba vs Fountain Gate Leo 25/09/2025 | Kikosi cha Simba Leo Dhidi ya Fountain Gate FC
Wekundu wa Msimbazi Simba SC leo watashuka dimbani kuwakabili Fountain Gate FC katika mchezo wa kwanza wa kuusaka ubabe wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu wa 2025/2026, baada ya misimu kadhaa ya kukwama mbele ya watani wao wa jadi Yanga SC.
Simba itaingia kwenye mchezo huu wakiwa na shauku kubwa ya kuanza kampeni za ligi kwa ushindi, hatua ambayo inaweza kuwa ishara ya kurejea kwao kwenye mbio za ubingwa.
Simba inatarajiwa kuingia uwanjani ikiwa na morali ya juu, licha ya msimu uliopita kumalizika kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga. Kocha Seleman Matola, ambaye amerudi rasmi kusimamia benchi la ufundi baada ya kuondoka kwa Fadlu Davids, amesisitiza umuhimu wa kikosi chake kuanza ligi kwa kupata alama tatu.
Matola alionekana mwenye kujiamini akibainisha kuwa changamoto za mabadiliko ya benchi la ufundi si jambo jipya kwa Simba, na kikubwa ni kuhakikisha wachezaji wanatekeleza malengo ya msimu. Kauli yake ni wazi kwamba Simba inalenga kuchukua ubingwa wa ligi, na mechi ya leo dhidi ya Fountain Gate ni hatua ya kwanza kuelekea safari hiyo.
Kwa upande wa wapinzani, Fountain Gate FC wanakabiliwa na wakati mgumu. Kikosi hicho kimejikuta kikiwa na wachezaji 14 pekee waliopo tayari kutokana na tatizo la kiufundi kwenye mfumo wa usajili wa kimataifa (TMS).
Changamoto hii imekumbusha tukio la misimu iliyopita, pale Kitayosce (sasa TRA United) iliposhindwa kuikamilisha idadi ya wachezaji na kulazimika kusalimu amri mapema dhidi ya Azam FC.
Kocha Denis Kitambi amekiri ugumu wa maandalizi kuelekea mechi hii, hasa kutokana na majeraha ya wachezaji wanne walioumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, ambao walipoteza kwa bao 1-0. Hata hivyo, Kitambi amesisitiza kuwa kikosi chake hakitashuka uwanjani kwa unyonge, badala yake kitaonyesha uwezo na kutumia nafasi chache zitakazojitokeza.
Kikosi cha Simba vs Fountain Gate Leo 25/09/2025
Kikosi rasmi cha Simba kitakachoshuka dimbani usiku wa leo dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kinatarajiwa kutangazwa rasmi majira ya saa 12:00 jioni.
Kwa mujibu wa maandalizi ya awali, wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza kama Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala, na Ellie Mpanzu wanatarajiwa kuanza katika mechi hii ya kwanza ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.
Mchezo huu unatarajiwa kuvutia hisia kubwa kutoka kwa mashabiki, ukizingatia presha iliyopo kwa Simba kuanza msimu kwa ushindi na changamoto zinazoiandama Fountain Gate kutokana na idadi ndogo ya wachezaji.
Mitazamo ya makocha
Kocha Matola amesisitiza kwamba anatarajia mchezo mgumu kutokana na ari ya Fountain Gate kuepuka kupoteza mechi ya pili mfululizo.
“Ligi ya Tanzania ni ngumu na bora, hakuna mechi rahisi. Lakini malengo yetu ni kuanza msimu kwa ushindi na tunaamini tuna nafasi kubwa ya kufanya hivyo,” alisema.
Kwa upande mwingine, Kitambi ameweka wazi kuwa presha kubwa ipo kwa Simba, ambao wengi wanawatarajia kushinda.
“Sisi tunaingia kucheza kwa malengo yetu, lakini bila shaka Simba ndiyo watakuwa kwenye presha ya kupata matokeo mazuri mbele ya mashabiki wao,” alisema.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania 2025/2026
- Matokeo ya Yanga vs Pamba Jiji Leo 24/09/2025
- Vilabu Bora Afrika 2025 (CAF Club Ranking 2025)
- Hat-Trick ya Mayele Yaipa Pyramids Ubingwa wa FIFA African-Asian-Pacific
- Ratiba ya NBC Premier league 2025/2026
- Serikali Yatoa Ufafanuzi Pamba Jiji Kufanya Mazoezi Gizani Uwanja wa Taifa
- Ratiba ya Mechi za Leo 24/09/2025
Leave a Reply