Kikosi cha Yanga vs Silver Strikers Leo 18/10/2025
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania, Yanga SC, leo watashuka dimbani kwa mara nyingine kupeperusha bendera ya taifa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAF Champions League). Wanajangwani hao watakuwa ugenini nchini Malawi, wakipambana na Silver Strikers katika mchezo muhimu wa raundi ya pili ya hatua za awali ya michuano hiyo.
Mchezo huu wa kukata na shoka unatarajiwa kuchezwa leo, tarehe 18 Oktoba 2025, kwenye Uwanja wa Bingu jijini Lilongwe, kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki (16:00 EAT).
Safari ya Yanga SC kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika
Yanga SC inaendelea kuonesha ubabe barani Afrika msimu huu baada ya kuanza kampeni zake kwa mafanikio makubwa. Klabu hiyo kutoka Jangwani haijapoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa msimu wa 2025/2026, ikiwa imeshinda mechi nne na kupata sare moja katika mashindano yote.
Safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa ngome imara, ikiongozwa na kipa Djigui Diarra pamoja na mabeki Ibrahim Bacca na Dickson Job, ambao hadi sasa hawajaruhusu bao hata moja. Upande wa ushambuliaji, Wanajangwani hao wamefunga mabao tisa, wakionyesha ufanisi mkubwa katika eneo la mbele.
Katika raundi ya kwanza ya michuano hii, Yanga iliiondoa Wiliete SC ya Angola kwa jumla ya mabao 5–0, ikishinda 3–0 ugenini na 2–0 nyumbani, matokeo yaliyodhihirisha uimara wa kikosi hicho chini ya benchi la ufundi la Romain Folz.
Hali ya Silver Strikers Kabla ya Mchezo
Kwa upande wa wenyeji, Silver Strikers walitinga hatua hii baada ya kuiondoa Elgeco PLUS ya Madagascar kwa faida ya bao la ugenini, baada ya kutoka 1-1 ugenini na 0-0 nyumbani. Ingawa matokeo yao ya hivi karibuni hayajawa mazuri wakiwa wameambulia sare mbili na kipigo kimoja katika mechi tatu zilizopita bado wanabaki kuwa wapinzani wenye uwezo mkubwa.
Silver Strikers inafundishwa na Kocha Peter Mgangira, na wachezaji wake muhimu ni pamoja na Uchizi Vunga, Levison Maganizo, George Chikooka, Maxwell Paipi, Dan Sandukira, Nickson Mwase, Stanie Davie, na Chinsisi Maonga. Eneo la kiungo limekuwa ngome yao kuu, ambapo Vunga na Maganizo wamekuwa wakicheza kwa nidhamu na ubunifu mkubwa.
Kikosi cha Yanga vs Silver Strikers Leo 18/10/2025
Mashabiki wengi wanatazamia kwa hamu kuona orodha ya wachezaji ambao Kocha Folz atawapanga katika mchezo wa leo. Kwa kawaida, katika michezo ya kimataifa ya CAF, kikosi cha kwanza hutangazwa rasmi saa moja kabla ya mchezo kuanza.
Hivyo basi, kikosi rasmi cha Yanga SC dhidi ya Silver Strikers Leo 18/10/2025 kitapangwa na kuthibitishwa na benchi la ufundi kabla ya kipenga cha kwanza. Habariforum itakuletea mara moja kikosi kamili cha Yanga pindi kitakapotangazwa rasmi.
Wachezaji wakuangaliawa na Mbinu za Uwanjani
Upande wa Yanga, eneo la kiungo limekuwa na ubora wa hali ya juu likiongozwa na Aziz Andabwile, ambaye ameonesha kiwango cha kuvutia tangu kuwasili kwa Kocha Romain Folz.
Wengine wanaotarajiwa kutoa mchango mkubwa ni Mohamed Doumbia, Balla Moussa Conte, Duke Abuya, na Mudathir Yahya, huku Pacome Zouzoua akitarajiwa kutoa msaada mkubwa katika eneo la ushambuliaji kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkali katika eneo la kiungo, ambapo pande zote mbili zinategemea ubunifu na nidhamu ya wachezaji wao wa kati. Kwa kuzingatia historia na rekodi za hivi karibuni, Yanga inaonekana kuwa na ubora wa juu zaidi, hasa katika matumizi ya nafasi na uthabiti wa ulinzi.
Kauli ya Kocha Msaidizi Patrick Mabedi
Kocha Msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, ambaye ni raia wa Malawi, amesema mechi hii ni maalum kwake kwa sababu anarejea nyumbani kupambana na timu ya nchi yake.
“Mechi hii ni muhimu sana, ninarudi nyumbani tukicheza na Silver Strikers ambayo ni timu ya nyumbani. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na kufuzu hatua inayofuata,” alisema Mabedi.
Mabedi, ambaye aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Malawi, amesema anawafahamu vizuri baadhi ya wachezaji wa Silver Strikers, akiwemo wale aliowahi kuwafundisha katika kikosi cha taifa cha vijana chini ya miaka 20.
“Ninajua udhaifu na nguvu zao, lakini mwisho wa yote tunapaswa kupambana ili kupata matokeo mazuri,” aliongeza.
Hata hivyo, alionya kwamba licha ya wapinzani wao kutokuwa na matokeo mazuri hivi karibuni, hawapaswi kudharauliwa.
“Katika soka, timu inayodhaniwa dhaifu inaweza kutoa ushindani mkubwa dhidi ya timu kubwa. Hivyo, tunapaswa kuwa makini na kujituma zaidi,” alisema.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Silver Strikers vs Yanga Sc Leo 18/10/2025 Saa Ngapi?
- Timu Zilizofuzu Kombe la Dunia 2026
- Msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar PBZ 2025/2026
- Majina Ya Usaili Kusimamia Uchaguzi 2025 Jimbo La Temeke, Mbagala na Chamazi
- Pacome Anukia Kombe la Dunia Baada ya Ushindi 7-0 Dhidi ya Shelisheli
- Zimbabwe Yainyima Nafasi Afrika Kusini Kufuzu Kombe la Dunia
- Kaizer Chiefs Ya Thibitisha Kuachana na Kocha Nasreddine Nabi
Leave a Reply