Klabu ya Liverpool Yamwaga Mamilioni Kumnasa Florian Wirtz
Klabu ya Liverpool imethibitisha kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji mahiri kutoka Ujerumani, Florian Wirtz, kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 116. Katika dili hilo, Majogoo wa Anfield wamelipa pauni milioni 100 kama kiasi cha awali huku pauni milioni 16 zikitarajiwa kulipwa baadaye kama nyongeza.
Uhamisho huu umevunja rekodi ya awali ya usajili ghali zaidi katika historia ya Liverpool, iliyokuwa ikishikiliwa na Darwin Núñez aliyesajiliwa kutoka Benfica kwa pauni milioni 85 mwaka 2022. Vilevile, mkataba huu unaweka rekodi mpya ya uhamisho wa juu zaidi katika Ligi Kuu England, ukiipiku ada ya pauni milioni 115 iliyolipwa na Chelsea kwa ajili ya Moisés Caicedo mwaka jana.
Mkataba wa Miaka Mitano Mpaka 2030
Florian Wirtz, mwenye umri wa miaka 22, ametia saini mkataba wa muda mrefu na Liverpool utakaomuweka Anfield hadi mwaka 2030. Mchezaji huyo alikamilisha vipimo vya afya katika kituo cha mazoezi cha klabu hiyo siku ya Ijumaa kabla ya kusaini rasmi mkataba wake mpya. Kabla ya usajili huu, rekodi ya usajili ya Liverpool ilikuwa ni pauni milioni 75 iliyotumika kumnasa beki Virgil van Dijk kutoka Southampton mwaka 2018.
Ndoto Kubwa za Wirtz Anfield
Akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi, Florian Wirtz alieleza matarajio yake makubwa akiwa Anfield:
“Ninataka kushinda kila kitu kila mwaka. Lakini kwanza ni lazima tufanye kazi yetu vizuri.”
Wirtz, ambaye namba yake ya jezi itatangazwa baadaye katika majira ya joto, aliongeza kuwa malengo yake makuu ni kusaidia Liverpool kutwaa tena taji la Ligi Kuu England na pia kufika mbali zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Safari Mpya Kutoka Bundesliga Mpaka Premier League
Wirtz anakuja Liverpool baada ya kung’ara akiwa Bayer Leverkusen, ambapo alifunga mabao 57 katika mechi 197. Alichanua zaidi msimu wa 2024/25 ambapo alicheza mechi 31 za Bundesliga, 23 kati ya hizo akitokea kama kiungo mshambuliaji (namba 10). Ingawa mara kwa mara anapendelea kucheza upande wa kushoto, uwezo wake wa kushambulia kutoka katikati ni wa kipekee.
Mchezaji huyo alifanya historia mwaka 2020 kwa kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye Bundesliga dhidi ya Bayern Munich, akiwa na umri wa miaka 17 na siku 19 tu baada ya kuanza kucheza ligi kuu. Tangu wakati huo, ametoa pasi 44 za mabao – idadi kubwa kwa mchezaji mwenye umri chini ya miaka 30 katika Bundesliga.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa soka la Ujerumani, Raphael Honigstein, Liverpool wamepata mchezaji “aliyekamilika” ambaye ataongeza ubora mkubwa katika kikosi. Honigstein anaeleza kuwa Wirtz ni nyota mwenye uwezo mkubwa, anayejua vyema presha ya mashindano makubwa kutokana na uzoefu wake na Leverkusen pamoja na timu ya taifa ya Ujerumani.
Aidha, licha ya umri wake mdogo, Wirtz ni mchezaji mwenye ushawishi mkubwa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo. Constantin Eckner, mwandishi wa kandanda la Ujerumani, anaeleza kuwa:
“Tangu mwanzo wa taaluma yake Bundesliga, alionekana kama kiongozi wa asili. Si mzungumzaji sana, lakini uwepo wake unahisiwa.”
Mapendekezo ya Mhariri:
- Viingilio Simba SC vs Kagera Sugar 22/06/2025
- Viingilio Yanga VS Dodoma Jiji 22/06/2025
- Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
- Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
- Kaizer Chiefs Wavamia Dili la Yanga SC Kunasa Saini ya Percy Tau
- Mashujaa FC Yaanza Harakati za Kumsajili Beki wa Simba SC
- Mamelodi Yaanza Kwa Ushindi wa 1-0 Dhidi ya Ulsan HD Kombe la Dunia
Leave a Reply