Nabi Atoa Angalizo Simba, Asema Yanga Ni Balaa! Chivaviro Asimulia
Yanga SC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wameendelea kuonyesha nia yao ya kutawala soka la ndani na kimataifa kwa kuichapa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mabao 4-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa nchini humo. Ushindi huu mkubwa umeacha kocha wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, akitoa angalizo kwa watani wa jadi wa Yanga, Simba SC, huku mshambuliaji wa Chiefs, Ranga Chivaviro, akielezea jinsi walivyopata tabu mbele ya Wanajangwani hao.
Nabi: Yanga Wamebadilika Sana
Nabi, ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga, alikiri kwamba kilichoomuumiza zaidi kwenye mechi hiyo ni ukubwa wa kipigo walichopata, lakini akasema walistahili. Alieleza kuwa Yanga imebadilika sana na sasa inaweka presha kubwa kwa wapinzani wanapokuwa na mpira, jambo ambalo liliwafanya vijana wake wengi kushindwa kuhimili.
“Timu yetu ina wachezaji wadogo kidogo ambao hawakuwa tayari kukutana na ugumu wa namna ile,” alisema Nabi. “Ukiangalia unaona namna ambavyo Yanga ilipokuwa haina mpira iliweka presha kubwa kwetu na vijana kujikuta wanafanya makosa makubwa.”
Nabi aliongeza kuwa kitu ambacho imekutana nacho timu yake kinaweza kuikumba timu yoyote ndani na nje ya Tanzania msimu ujao ambayo haijajiandaa sawasawa kukutana na mbinu za namna hiyo za timu inayoweka presha kubwa kwa wapinzani wanapokuwa na mpira. Hii ni angalizo tosha kwa Simba, ambao watakutana na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii na baadaye kwenye ligi.
Chivaviro: Yanga Hawakutupa Nafasi
Mshambuliaji Ranga Chivaviro wa Kaizer Chiefs, ambaye aliwahi kuwindwa na Yanga, alisema Yanga iliwaweka kwenye wakati mgumu ambapo nidhamu yao wakati hawana mpira ilikuwa kitu kigumu kwao kuweza kuhimili.
“Ilikuwa ngumu kwetu, ni kama hawakutupa nafasi ya kujipanga wakati tukiwa tuna mpira,” alisema Chivaviro. “Walikuwa wanalazimisha haraka tuupoteze uwe chini yao nadhani ndio silaha waliyoitumia kutengeneza ushindi kama ule.”
Yanga Yaonyesha Makali Ziara ya Afrika Kusini
Ziara ya Yanga Afrika Kusini imekamilika kwa timu hiyo kuonyesha kiwango kizuri ambapo licha ya kucheza mechi tatu ikafunga mabao sita huku ikipoteza mchezo mmoja pekee. Ushindi huu mkubwa dhidi ya Kaizer Chiefs unaashiria kuwa Yanga wako tayari kutetea taji lao la ligi na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Agosti 8: Haji Manara Awaonya Simba SC Dhidi ya Kuleta Timu Uwanjani
- Yusuph Kagoma kuikosa Kariakoo Dabi
- Simba SC Yafunga Pre-season kwa Ushindi
- Aziz Ki Atawazwa Mchezaji Bora Fainali Toyota Cup 2024
- Yanga Sc Wabeba Kombe la Toyota Cup 2024
- Hizi Apa Picha Za Jezi Mpya Ya Yanga Sc 2024/2025
- Jezi Mpya Za Yanga 2024/2025
- Hivi Apa Vituo Vya Kununua Tiketi Simba Day 2024
Weka Komenti