Ousmane Dembélé Ashinda Tuzo ya Ballon d’Or 2025
Nyota wa Paris Saint-Germain (PSG), Ousmane Dembélé ameibuka mshindi wa tuzo ya kifahari ya Ballon d’Or 2025, akimshinda chipukizi wa Barcelona, Lamine Yamal, aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika fainali ya kinyang’anyiro hicho.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo za kila mwaka imefanyika jijini Paris, Ufaransa, ambapo mastaa wa soka duniani walipewa heshima zao kutokana na mafanikio ya msimu wa 2024/2025.
Kiwango Bora cha Dembélé Kilivyompa Ubingwa
Kitu kilichomuinua Dembélé hadi kushinda tuzo hii ni kiwango bora alichoonesha akiwa PSG. Katika msimu wa 2024/2025, Dembélé alifunga mabao 35 na kutoa pasi 14 za mabao katika michezo 53 ya mashindano tofauti, akibeba jukumu kubwa katika mafanikio ya klabu yake. Mchango wake ulichangia PSG kutwaa mataji manne makubwa, matatu yakiwa ya ndani ya Ufaransa na moja la kimataifa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Zaidi ya hapo, Dembélé aliendelea kung’ara kwa kufunga penalti muhimu katika ushindi wa mikwaju ya penalti 4–3, uliowapa PSG taji la UEFA Super Cup mwaka huu.
Washindi Wengine wa Tuzo za Ballon d’Or 2025
Licha ya kukosa nafasi ya kwanza, Lamine Yamal hakutoka mikono mitupu, kwani alitunukiwa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ballon d’Or 2025, kutokana na mchango wake wa kipekee akiwa na Barcelona.
Kwa upande wa mfungaji bora, Viktor Gyökeres alibeba tuzo hiyo baada ya kupachika mabao 54 katika mechi 52 akiwa na Sporting Lisbon msimu uliopita, kiwango kilichompa heshima kubwa barani Ulaya.
Tuzo ya Kipa Bora ilienda kwa Gianluigi Donnarumma wa Manchester City, huku PSG ikitajwa rasmi kuwa Timu Bora ya Mwaka (wanaume). Hali kadhalika, kocha wa PSG, Luis Enrique, alishinda Tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka (wanaume).
Kwa upande wa wanawake, Aitana Bonmatí wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania ameendelea kutamba baada ya kushinda Ballon d’Or ya Mchezaji Bora wa Dunia kwa mara ya tatu mfululizo, na kuweka rekodi mpya ya historia ya mpira wa miguu wa wanawake.
Vilevile, Vicky López wa Barcelona alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi (wanawake), huku Arsenal Women wakichaguliwa kuwa Timu Bora ya Wanawake 2025. Kwa upande wa makocha, Sarina Wiegman wa England ameibuka Kocha Bora wa Wanawake wa Mwaka, na Ewa Pajor wa Barcelona akatwaa Tuzo ya Mfungaji Bora Wanawake.
Aidha, Anna Hampton wa Chelsea alinyakua Tuzo ya Kipa Bora Wanawake Ballon d’Or 2025.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Mechi za Leo 22/09/2025
- Matokeo ya Gaborone United vs Simba leo 20/09/2025
- Hiki Apa Kikosi cha Simba vs Gaborone United leo 20/09/2025
- Viwango Vya FIFA Duniani 2025 (FIFA Rankings)
- Taifa Stars Yashuka Nafasi Nne Katika Orodha Mpya ya Viwango vya FIFA
- Benfica Yampa Mourinho Kibarua cha Kuiongoza kwa Miaka Miwili
- Yanga Yaanza Msimu wa Ligi ya Mabingwa Kwa Ushindi wa 3-0
Leave a Reply