Pamba Jiji FC Yamtambulisha Francis Baraza Kama Kocha Mkuu 2025/2026

Pamba Jiji FC Yamtambulisha Francis Baraza Kama Kocha Mkuu 2025/2026

Timu ya Pamba Jiji FC ya jijini Mwanza imemtambulisha rasmi Francis Baraza kuwa Kocha Mkuu kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2025/2026, hatua inayodhihirisha dhamira ya klabu hiyo kuimarisha safu ya benchi la ufundi na kuleta ushindani mkubwa katika ligi.

Baraza, ambaye ni raia wa Kenya na mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na kuchukua nafasi ya aliyekuwa kocha, Fred Felix Minziro, ambaye alihudumu msimu uliopita.

Akimtambulisha kocha huyo mpya, Mwenyekiti wa Pamba Jiji FC, Bhiku Kotecha, alieleza kuwa Baraza amekabidhiwa timu kwa uhuru kamili wa kufanya maamuzi ya kiufundi, huku uongozi ukiahidi kutoa ushirikiano pasipo kuingilia mipango ya benchi la ufundi.

“Tumemwambia Mwalimu sisi uongozi hatutamuingilia katika mipango yake ya timu wala kumpangia cha kufanya; tunachotaka ni atufanyie kazi tupate matokeo,” alisema Kotecha.

Pamba Jiji FC Yamtambulisha Francis Baraza Kama Kocha Mkuu 2025/2026

Safu Mpya ya Benchi la Ufundi

Katika mchakato wa maandalizi ya msimu ujao, Pamba Jiji FC pia imetangaza safu mpya ya benchi la ufundi litakaloongozwa na Baraza. Atasaidiana na Temi Felix kama Kocha Msaidizi, John Waw akiwa Kocha wa Makipa, Shaban Kado (Kocha Msaidizi wa Makipa), na George Aaron ambaye atahudumu kama Kocha wa Viungo. Safu hii imeundwa kwa lengo la kuimarisha mbinu za kiuchezaji na kuhakikisha timu inapata matokeo chanya msimu mzima.

Uzoefu na Maono ya Kocha Francis Baraza

Francis Baraza ana historia ndefu na tajiriba ya kipekee katika soka la Tanzania, akiwa tayari ameinoa Biashara United (Mara), Kagera Sugar (Kagera), Dodoma Jiji (Dodoma) na Tanzania Prisons (Mbeya). Uzoefu huu unampa faida ya kulifahamu vyema soka la ndani na wachezaji wake, jambo ambalo linaongeza matarajio makubwa kwa mashabiki wa Pamba Jiji FC.

Baraza amesema anajiamini kwa kiwango chake cha uzoefu na anafahamu vyema kikosi cha sasa cha Pamba Jiji FC, tayari amepokea orodha ya wachezaji na ameanza kuwafanyia tathmini.

“Najua hii ni kazi ngumu lakini naamini tukishikana pamoja, matokeo yatapatikana na timu itabadilika,” alisema. Aidha, alibainisha kuwa ana lengo la kuiweka Pamba Jiji FC katika nafasi tano za juu kwenye msimamo wa ligi msimu ujao.

Kocha Baraza amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema na usajili wa wachezaji kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu. Ameomba uongozi kuhakikisha mchakato wa usajili unakamilika mapema ili kuwezesha maandalizi ya kikosi kuanza kwa wakati.

“Lazima tushikane sisi Mwanza, tukiweza kufanya kazi yetu vizuri kwa kushirikiana, Pamba ina uwezo wa kumaliza katika nafasi tano bora, hilo naliona,” alisisitiza.

Katika hotuba yake, Baraza alitoa heshima kwa mtangulizi wake, Fred Minziro, akisema kuwa walishawahi kufanya kazi pamoja na kumtambua kama mwalimu aliyetoa mchango mkubwa katika kuifikisha Pamba Jiji FC Ligi Kuu. Aliahidi kuendeleza mazuri aliyoyaacha Minziro ili kuijenga timu imara na yenye ushindani mkubwa.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. CV Ya Rushine De Reuck Beki Mpya wa Simba 2025/2026
  2. Simba SC Yasaini Mkataba wa Sh20 Bilioni na Betway Kama Mdhamini Mkuu
  3. Wachezaji Wapya wa Yanga 2025/2026
  4. CV ya Moussa Balla Conte Mchezaji Mpya wa Yanga Sc 2025/2026
  5. Cv ya Romain Folz Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026
  6. Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
  7. Rashford Kuvaa Jezi Namba 14 Barcelona
  8. Serikali Yaahidi Sh1 Bilioni kwa Taifa Stars Wakitwaa Kombe la CHAN 2024
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo