Simba SC Yakata Tiketi Ligi ya Mabingwa Afrika 2025-2026 Baada ya Kufikisha Pointi 66

Simba SC Yakata Tiketi Ligi ya Mabingwa Afrika 2025 2026

Simba SC Yakata Tiketi Ligi ya Mabingwa Afrika 2025-2026

Dar es Salaam, Mei 8, 2025 — Klabu ya Simba SC imejihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2025/2026, baada ya kufikisha pointi 66 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote iliyo chini yake kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Hii ni baada ya ushindi wa kishindo wa mabao 5-1 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ulioanza kwa spidi na ushindani mkubwa, mshambuliaji Jean Charles Ahoua aliibuka shujaa kwa kufunga mabao matatu (hat trick) dakika ya 16, 37 na 52. Mabao mawili kati ya hayo yalitokana na mipira ya adhabu, akionyesha uwezo mkubwa wa kutumia nafasi za kutenga. Bao lake la kwanza lilifungwa kupitia mkwaju wa penalti baada ya Joshua Mutale kuchezewa faulo na mchezaji wa Pamba Jiji, Zabona Mayombya.

Pamba Jiji walijaribu kurejea mchezoni kwa mashambulizi kupitia kwa mshambuliaji wao Mathew Tegis, lakini safu ya ulinzi ya Simba chini ya uongozi wa kipa Moussa Camara ilidhibiti vema hatari zote. Hata hivyo, walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 88 kupitia kwa Tegis, ambaye sasa amefunga katika mechi tano mfululizo.

Katika dakika ya 37, Simba waliongeza bao la pili kupitia mpira wa adhabu uliopigwa moja kwa moja na Ahoua nje kidogo ya eneo la hatari, baada ya Mutale kufanyiwa faulo. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0, huku mwamuzi Shomari Lawi akitoa jumla ya kadi tatu za njano kwa wachezaji wa timu zote.

Simba SC Yakata Tiketi Ligi ya Mabingwa Afrika 2025-2026 Baada ya Kufikisha Pointi 66

Mabadiliko ya Kikosi Yaleta Tija

Kipindi cha pili kilianza kwa mabadiliko kadhaa ya wachezaji. Pamba Jiji walimtoa Paulini Kasindi na kumuingiza Saleh Masoud, huku Simba wakimpa nafasi Che Fondoh Malone badala ya Abdulrazack Hamza. Dakika ya 52, Ahoua alikamilisha hat trick yake kwa kichwa akitumia krosi ya Ellie Mpanzu, ambaye sasa ana jumla ya asisti tatu msimu huu.

Mabadiliko zaidi yaliendelea kufanyika, ambapo Simba waliwapumzisha wachezaji kama Shomari Kapombe, Jean Charles Ahoua, na Fabrice Ngoma, nafasi zao zikichukuliwa na Kibu Denis, Valentine Nouma na Debora Mavambo mtawalia. Kwa upande wa Pamba Jiji, kocha Fred Felix ‘Minziro’ aliingiza wachezaji wapya kama Samson Madeleke, Hamadi Majimemgi na Deus Kaseke, lakini bado haikusaidia kubadili matokeo.

Simba waliongeza mabao mawili dakika za lala salama kupitia kwa Leonel Ateba katika dakika ya 83 na 85, ambaye sasa amefikisha jumla ya mabao 12 kwenye msimu huu wa ligi.

Ahoua Aongoza Orodha ya Wafungaji

Hat trick ya Ahoua imemrejesha kileleni mwa chati ya wafungaji akiwa na mabao 15, akimzidi mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, mwenye mabao 13. Kabla ya mchezo huu, Ahoua alikuwa na mabao 12 lakini alizidiwa na Mzize wakati Simba ikishiriki mechi za kimataifa.

Ahoua pia anaongoza katika ufungaji wa penalti, akiwa amepachika wavuni zote sita kati ya sita alizopiga. Simba SC ndio timu iliyopata penalti nyingi zaidi msimu huu (13), ambapo Ateba naye amefunga sita kati ya saba alizopiga.

Camara na Vita ya Clean Sheet

Kipa wa Simba, Moussa Camara, alipoteza nafasi ya kupata clean sheet ya 17 baada ya kuruhusu bao la Mathew Tegis dakika za mwisho. Hadi sasa, Camara ana clean sheet 16 katika mechi 23 alizocheza, sawa na dakika 2,070. Ili avunje rekodi msimu huu, anahitaji clean sheet tatu katika mechi tano zilizosalia.

Kwa sasa, Camara anaongoza mbele ya Djigui Diarra wa Yanga mwenye clean sheet 14 katika mechi 20. Hata kama Diarra atatoka bila kuruhusu bao katika mechi zake zote nne zilizobaki, hatoweza kumfikia Camara iwapo huyu wa Simba atapata clean sheet tatu zaidi.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Yanga Yashikilia Msimamo wa Kutocheza Dabi Licha Ya Majibu ya CAS
  2. Simba Yaitandika JKT na Kujiweka Kwenye Njia ya Ligi ya Mabingwa
  3. Matokeo JKT Tanzania vs Simba Leo 05/05/2025
  4. Sababu 3 Zilizofanya CAS Kuitupilia Mbali Kesi ya Yanga
  5. Shauri la Yanga CAS Lapigwa Chini, Kariakoo Derby kupangiwa Tarehe
  6. Kipagwile Aibuka Mchezaji Bora Ligi Kuu April 2025, Ambwaga Pacome
  7. Guardiola Atangaza Kupumzika Ukocha Baada ya Mkataba Wa Man City Kuisha
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo