Simba SC Yasaini Mkataba wa Sh20 Bilioni na Betway Kama Mdhamini Mkuu
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wameandika historia mpya kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Shilingi bilioni 20 na kampuni ya kimataifa ya ubashiri wa michezo, Betway, kama mdhamini mkuu wa klabu hiyo.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo ilifanyika Jumanne, Julai 29, 2025 jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua rasmi ya kuhitimisha ushirikiano uliokuwepo kati ya Simba na mdhamini wao wa zamani, M-Bet.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Bi. Zubeda Sakuru, udhamini huu ni sehemu ya mkakati mpana wa klabu hiyo kujiimarisha na kuwa taasisi ya kisasa inayojitegemea kifedha, huku ikiweka malengo ya kuwa klabu namba moja barani Afrika.
“Mkataba huu unakwenda kuleta mapinduzi kwenye mchezo wa soka hapa Tanzania na unaongeza nguvu katika dhamira yetu ya kuifanya Simba kuwa klabu bora zaidi Afrika,” alieleza Sakuru.
Simba SC na Dhamira ya Kuinua Brand
Sakuru aliongeza kuwa ndani ya Bodi ya Simba, kipaumbele ni kuhakikisha chapa ya klabu inazidi kupanda thamani kila siku, jambo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki wa timu hiyo. “Nguvu kubwa ya Simba ni mashabiki wake. Ndiyo maana wadhamini wanajitokeza kuwekeza. Tunataka kuona Simba inazidi kuwa na ushawishi ndani na nje ya Tanzania,” alisema.
Mkataba huu wa Sh20 bilioni unafuatia mkataba wa awali na M-Bet, ambao ulisainiwa Agosti 1, 2022 kwa muda wa miaka mitano ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 26, milioni 168 na elfu tano. Hata hivyo, Simba imeamua kuingia katika ushirikiano mpya na Betway kwa matarajio ya kuimarisha misingi ya kifedha na kiutendaji ndani ya klabu.
Betway Yajitambulisha Rasmi
Kwa upande wa kampuni ya Betway, Mkuu wa Udhamini Afrika, Jason Shield, alisema kuwa wamefuatilia maendeleo ya Simba SC kwa zaidi ya miaka sita, na kwa sasa wamevutiwa na mwelekeo na ukubwa wa klabu hiyo. “Simba ni timu kubwa Afrika. Ushirikiano huu ni zaidi ya udhamini wa kawaida; tunataka kuona faida kwa pande zote mbili,” alisema Shield.
Shield alieleza kuwa uzoefu wa Betway katika kushirikiana na vilabu vikubwa duniani utakuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha mafanikio ya mkataba huu. “Tutatumia uzoefu wetu wa kimataifa kuhakikisha ushirikiano huu unaenda mbali zaidi ya udhamini wa kawaida,” alisisitiza.
Naye Meneja Uendeshaji wa Betway Tanzania, Jimmy Masaoe, alibainisha kuwa mashabiki wa Simba SC wategemee huduma bora, kwani kampuni yao imejipanga kuwahudumia kikamilifu. “Tumeandaa huduma mbalimbali mahsusi kwa mashabiki wa Simba. Betway ni kampuni ya kimataifa inayotoa huduma saa 24 kwa siku,” alieleza Masaoe.
Wito kwa Uwajibikaji na Uwazi
Akizungumza kwa niaba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Makamu wa Kwanza wa Rais, Athuman Nyamlani, aliipongeza Simba SC kwa hatua hiyo kubwa ya kimaendeleo, akisema ni matokeo ya ubora unaozidi kuongezeka kwenye ligi ya Tanzania. “Ni hatua kubwa sana. Lakini tunasisitiza matumizi bora na yenye uwazi wa fedha hizi za udhamini ili kuongeza imani ya wadhamini wengine,” alisema Nyamlani.
Aidha, Nyamlani aliwataka viongozi wa klabu kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kuimarisha kikosi, miundombinu, na mifumo ya kitaasisi ndani ya Simba SC, kwa kuwa mafanikio ya sasa ya udhamini ni msingi wa mikataba mikubwa zaidi siku zijazo.
Mjumbe wa Bodi ya Simba SC, Salim Muhene maarufu kama “Try Again”, aliwataka mashabiki wa Simba kuonyesha mshikamano na kampuni ya Betway kama ishara ya kuunga mkono maendeleo ya klabu yao. “Tuwape ushirikiano Betway ili wapate kile wanachokitafuta, na siku zijazo tukumbatiwe na mikataba mikubwa zaidi,” alisema Muhene.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Wachezaji Wapya wa Yanga 2025/2026
- CV ya Moussa Balla Conte Mchezaji Mpya wa Yanga Sc 2025/2026
- Cv ya Romain Folz Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026
- Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
- Rashford Kuvaa Jezi Namba 14 Barcelona
- Serikali Yaahidi Sh1 Bilioni kwa Taifa Stars Wakitwaa Kombe la CHAN 2024
- Tetesi za Usajili Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2025/2026
- Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
Leave a Reply