Simba Yathibitisha Kumtoa Omary Omary kwa Mkopo kwenda Mashujaa FC
Klabu ya Simba SC imethibitisha rasmi kumtoa kiungo wake wa kati, Omary Omary, kwa mkopo kwenda Mashujaa FC kwa ajili ya msimu wa mashindano wa 2025/26. Kiungo huyo anarejea tena katika klabu yake ya zamani baada ya takribani mwaka mmoja na nusu tangu alipojiunga na Wekundu wa Msimbazi mnamo Juni 22, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Simba SC, uhamisho huu wa mkopo umelenga kumpa mchezaji huyo nafasi ya kupata muda zaidi wa kucheza, kuimarisha kiwango chake, na kujifunza kupitia mashindano ya mara kwa mara.
Klabu hiyo imeeleza kuwa hii ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi, na kuwajengea mazingira bora ya ushindani kabla ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Omary Omary Arejea Mashujaa FC kwa Matarajio Mapya
Omary, ambaye ni kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kusukuma mashambulizi kutoka katikati ya uwanja, alisajiliwa na Simba SC kwa mkataba wa miaka miwili. Hata hivyo, ndani ya kipindi hicho, amekuwa akikosa nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkali uliopo ndani ya timu.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba SC, uamuzi wa kumtoa kwa mkopo umetokana na ukweli kwamba mchezaji huyo hakuweza kuendana na kasi ya timu na alishindwa kuonyesha ushindani kwenye nafasi aliyokuwa akiwania.
“Omary ni miongoni mwa nyota ambao wanatolewa kwa mkopo kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya timu yetu, akishindwa kuonyesha ushindani kwenye nafasi anayocheza. Hivyo tunamwondoa kupisha nyota wengine,” kilieleza chanzo hicho.
Omary Omary Athibitisha Hatua Hiyo: “Ni Wakati wa Kuanza Upya”
Katika mahojiano na gazeti la Mwanaspoti, Omary Omary mwenyewe alithibitisha taarifa hizo kuwa ni za kweli, na kufichua kuwa yeye ndiye aliyeomba kurejea Mashujaa FC baada ya kubaini kuwa hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Simba SC.
“Taarifa za mimi kutolewa kwa mkopo ni za kweli na natarajia kurudi Mashujaa kama mambo yataenda vizuri. Sikuwa na nafasi ya kuonyesha uwezo wangu, lakini bado naamini nina nafasi ya kufanya vizuri kwenye timu nitakayopenda,” alisema Omary.
Aidha, aliweka wazi kuwa mazingira ya ushindani ndani ya Simba SC yalikuwa ya juu sana, huku timu hiyo ikiwa na malengo makubwa ya kutwaa mataji, jambo lililomlazimu kufikiria hatua mpya ya kimaendeleo.
“Ushindani ulikuwa mkubwa na nilikuwa kwenye timu yenye presha ya matokeo. Nafikiri huu ni muda sahihi wa mimi kurudi kujaribu maisha mengine. Naamini nina nafasi ya kufanya makubwa zaidi,” aliongeza.
Mkakati Mpana wa Simba SC Kuwatoa Kwa Mkopo Wachezaji Waiopata Nafasi
Hatua ya kumtoa Omary kwa mkopo ni sehemu ya mchakato mpana unaofanywa na Simba SC kuelekea msimu mpya.
Klabu hiyo imekuwa katika mazungumzo na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwakopesha wachezaji wao ambao hawajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Miongoni mwa wachezaji wengine wanaotarajiwa kutolewa kwa mkopo ni Edwin Balua, anayetajwa kujiunga na Enosis Athletic Union ya Cyprus, pamoja na Valentino Mashaka. Wakati huo huo, wachezaji kama Fabrice Ngoma, Valentino Nouma, na Kelvin Kijiri wamemalizana na klabu hiyo na wanajiandaa kutimkia timu nyingine.
View this post on Instagram
Mapendekezo Ya Mhariri:
- Kibabage Akaribia Kujiunga Singida Bs Baada ya Kumaliza Mkataba Yanga
- Simba Yamalizana na Kiungo Balla Moussa Conte Kutokea CS Sfaxien
- Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026: Siri Yafichuka Jangwani!
- Singida BS Yamnyatia Kipa wa Simba Hussein Abel Baada ya Kumaliza Mkataba
- Wachezaji 6 wa KMC Wasubiri Hatima Yao Kufuatia Mikataba Kumalizika
- Kennedy Musonda Atimkia Israel Baada ya Kumaliza Mkataba na Yanga
- Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
Leave a Reply