Singida BS Yavunja Benchi Zima la Ufundi Baada ya Kipigo Dhidi TRA United
Klabu ya Singida Black Stars imethibitisha rasmi kuvunja benchi zima la ufundi la timu hiyo iliyokuwa chini ya kocha Othmen Najar kuanzia leo, Aprili 05, 2026, ikiwa ni muda mfupi baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa TRA United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. Uamuzi huo umetangazwa kupitia taarifa ya uongozi wa klabu hiyo, ukielezwa kuwa umetokana na mwenendo usioridhisha wa matokeo katika michezo ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kurekebisha mwelekeo wa timu huku ikijiandaa na michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara. “Uongozi wa Klabu ya Singida Black Stars unatangaza rasmi kuvunjwa kwa benchi zima la ufundi la timu kuanzia leo, tarehe 05 Aprili 2026. Uamuzi huu umefikiwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika kipindi cha hivi karibuni,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa klabu hiyo itakuja na mpango wa muda mfupi kwa kutangaza benchi la ufundi la mpito litakaloisimamia timu wakati maandalizi ya michezo mingine yakiendelea.
Mchezo dhidi ya TRA United Ulivyokua
Katika mchezo huo uliochezwa Arusha, TRA United walionyesha ushindani mkubwa tangu dakika za mwanzo. Bao la kwanza lilipatikana mapema dakika ya 10 baada ya beki wa Singida, Abdallah Kheri Sebo, kujifunga na kuiweka timu yake kwenye wakati mgumu.
Shinikizo liliendelea kwa Singida huku TRA wakiongeza bao la pili dakika ya 40 kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Christopher Tebandeje, kufuatia tukio la faulo lililotambuliwa ndani ya eneo la hatari.
Singida walipata nafasi ya kurejea mchezoni baada ya kupewa penalti kufuatia beki wa TRA United, Chamoe Karaboue, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, kiungo mshambuliaji Lamine Jarjou alishindwa kuitumia nafasi hiyo baada ya kupiga mpira nje, hali iliyoifanya timu hiyo kumaliza mchezo bila kufumania nyavu.
Mwenendo wa Hivi Karibuni wa Singida Black Stars
Matokeo ya mchezo huo yanaongeza presha kwa Singida Black Stars, ambayo sasa imepoteza michezo minne kati ya sita iliyocheza hivi karibuni. Katika kipindi hicho, timu hiyo ilifanikiwa kushinda michezo miwili pekee dhidi ya Tanzania Prisons (2-1) na Mbeya City (4-1).
Hata hivyo, ilipoteza michezo dhidi ya Simba (2-1), Yanga (3-0), Azam (2-1) na sasa TRA United (2-0), hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa uamuzi wa kuvunja benchi la ufundi.
Nafasi ya Singida Kwenye Msimamo wa Ligi
Licha ya matokeo hayo yasiyoridhisha, Singida Black Stars bado inashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 25. Tofauti ya pointi moja tu na Pamba Jiji iliyo nafasi ya tano inaonyesha kuwa bado timu hiyo ina nafasi ya kurekebisha msimamo wake endapo itapata mwendelezo mzuri wa matokeo.
Mapendekezo ya Mhariri:








Leave a Reply