Taifa Stars yaichakaza Macau 6-0 FIFA Series

Taifa Stars yaichakaza Macau 6-0 FIFA Series

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imepata ushindi mkubwa wa mabao 6-0 dhidi ya Macau katika michuano ya FIFA Series inayoendelea jijini Kigali, Rwanda, matokeo yaliyompa kocha Miguel Gamondi ushindi wake wa kwanza katika mechi za kimataifa tangu aanze kuinoa timu hiyo.

Ushindi huo unafuatia kipindi kigumu kwa Stars iliyokuwa imecheza mechi tano mfululizo bila ushindi, sawa na dakika 450 bila kupata matokeo chanya. Matokeo hayo pia yanakuja siku chache baada ya Stars kupoteza mechi ya ufunguzi ya michuano hiyo kwa bao 1-0 dhidi ya Liechtenstein.

Gamondi alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi kwa kubadili wachezaji 10 waliocheza mechi iliyopita, lakini mabadiliko hayo yalionekana kuipa timu uhai mpya, huku Stars ikitawala mchezo kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Taifa Stars yaichakaza Macau 6-0 FIFA Series

Katika kipindi cha kwanza, Taifa Stars ilionyesha ubora wake kwa kupiga mashuti 11, matano yakilenga lango. Bao la kwanza lilipatikana dakika ya 16 baada ya Amancio wa Macau kujifunga, kabla ya Bakari Mwamnyeto kuongeza la pili dakika ya 26. Mudathir Yahya alihitimisha kipindi cha kwanza kwa bao la tatu dakika ya 45.

Kipindi cha pili kilishuhudia kasi ile ile ya ushambuliaji, ambapo Paul Peter alifunga bao la nne dakika ya 56, Novatus Dismas akaongeza la tano dakika ya 74, na Allarakhia akahitimisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la sita dakika ya 87.

Kiungo Charles M’Mombwa alikuwa miongoni mwa wachezaji waliojitokeza zaidi katika mchezo huo, akihusika moja kwa moja na mabao matatu kati ya sita. Alichangia bao la kwanza lililojifungwa na Amancio na kutoa asisti kwa mabao ya Mudathir Yahya na Paul Peter ndani ya dakika 56 alizocheza.

Ushindi huo wa mabao 6-0 unatajwa kuwa miongoni mwa matokeo makubwa zaidi kwa Taifa Stars katika miaka ya hivi karibuni, na unaongeza matumaini mapya kwa kikosi hicho kuelekea mashindano yajayo.

Gamondi, ambaye aliiongoza Stars kwa mara ya kwanza katika fainali za Mataifa ya Afrika nchini Morocco akiwa kocha wa muda, aliweka historia kwa kufikisha timu hatua ya 16 bora licha ya kutoshinda mechi yoyote katika hatua ya makundi. Stars ilikusanya pointi mbili baada ya sare mbili za 1-1 dhidi ya Uganda na Tunisia, kabla ya kufungwa 2-1 na Nigeria.

Katika hatua ya 16 bora, Stars ilitolewa kwa kufungwa 1-0 dhidi ya wenyeji wa mashindano hayo, lakini mafanikio ya kufika hatua hiyo yalionekana kuwa hatua muhimu katika maendeleo ya soka la Tanzania.

Ushindi dhidi ya Macau pia ni ushindi wa pili kwa Taifa Stars katika michuano ya FIFA Series, baada ya awali kuifunga Mongolia mabao 3-0 katika mashindano yaliyofanyika Azerbaijan.

Kwa upande wa wafungaji, Novatus Dismas anaendelea kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi kwa Stars katika michuano hiyo, akiwa amefunga mabao mawili hadi sasa, likiwemo bao katika ushindi dhidi ya Macau.

Matokeo haya yanaipa Taifa Stars msingi mzuri wa kuendelea kujijenga kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika 2027, ambapo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zitakazoandaa mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Tanzania Football Team Player Squad: National Football Guide
  2. Diarra Afungiwa Mechi 3 na Kutozwa Milioni 2 kwa Utovu wa Nidhamu
  3. Ratiba ya Michezo ya Kimataifa Michuano ya FIFA Series 2026
  4. Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo