Yanga SC Kusherehekea Vikombe 5 Leo Jijini Dar – Paredi Kubwa Yatarajiwa
Dar es Salaam, Juni 30, 2025 – Klabu ya Yanga SC leo inatarajiwa kuliteka jiji la Dar es Salaam kwa shangwe kubwa, kufuatia maandalizi ya paredi ya kihistoria baada ya kutwaa jumla ya vikombe vitano msimu wa 2024/2025. Vikombe hivyo ni pamoja na ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA (Shirikisho la CRDB), Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, na Kombe la Toyota.
Timu hiyo yenye rekodi ya kutwaa ubingwa mara nyingi zaidi nchini, imetawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mfululizo, baada ya kumaliza msimu kwa alama 82 alama nne zaidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC, waliomaliza nafasi ya pili kwa alama 78. Mafanikio hayo yamethibitisha uimara wa kikosi hicho msimu huu, hali iliyoamsha shauku kubwa kwa mashabiki wake ambao leo wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kusherehekea ushindi huo wa kihistoria.
Paredi Kubwa Ya Kihistoria
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe, paredi ya leo itakuwa tofauti kabisa na ile ya misimu iliyopita. Safari hii, klabu hiyo imeongeza vituo vya kusimama ili kuwapa nafasi mashabiki wengi zaidi kushiriki kwenye shamrashamra hizo. Kamwe ameeleza kuwa paredi hiyo itaanza mara baada ya timu kutua Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, ikianzia rasmi katika maeneo ya Buguruni na kuelekea maeneo mbalimbali ya jiji.
Katika eneo la Msimbazi, ambako awali walikuwa wakisimama kwa muda wa dakika tano tu, msimu huu watakaa kwa zaidi ya saa tatu, hatua inayoonesha jinsi sherehe hizi zilivyopewa uzito mkubwa na viongozi wa klabu hiyo.
Mastaa Kuhutubia Taifa
Wakati wa kituo cha Msimbazi, wachezaji nyota wa Yanga SC akiwemo Clatous Chama, Israel Mwenda, na Jonas Mkude wanatarajiwa kusimama juu ya gari maalum na kuwahutubia mashabiki pamoja na Watanzania kwa ujumla. Hii ni hatua ya kipekee inayolenga kuonesha mshikamano baina ya klabu na mashabiki wake.
Kamwe amesema kuwa, licha ya changamoto zilizowakumba msimu huu, mshikamano na umoja wa ndani ya klabu umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo. “Siri yetu ni mshikamano. Viongozi waliaminiwa na mashabiki na walifanikiwa kutuvusha salama. Siamini kama kuna Mwanayanga atabaki nyumbani leo bila kushiriki kwenye sherehe hizi,” aliongeza.
Takwimu za Ubingwa
Msimu wa 2024/2025, Yanga SC imeonesha kiwango cha juu cha ushindani kwa kupoteza michezo miwili pekee dhidi ya Tabora United na Azam FC. Pia walitoka sare katika michezo miwili na kufunga jumla ya mabao 83 huku wakiruhusu mabao 10 pekee, hali inayoonesha uimara wa safu yao ya ushambuliaji na ulinzi.
Ushindi huo wa Kombe la FA ulifungwa rasmi jana, baada ya Yanga kuichapa Singida Black Stars kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB. Hii ilikuwa kama sahihi ya mwisho kwenye mafanikio yao makubwa ya msimu huu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Kikosi cha Yanga vs Singida Black Stars Leo 29/06/2025 Fainali ya CRDB
- Matokeo ya Yanga vs Singida Black Stars Leo 29/06/2025
- Ratiba ya Fainali ya CRDB Federation Cup 2025
- Chelsea Yajipanga Kuzima Moto wa Di Maria Katika Mechi ya Usiku Dhidi ya Benfica
- Simba Yavizia Saini ya Issa Fofana Nchini Ivory Coast Kama Mrithi wa Camara
- Ratiba ya CHAN 2024/2025 | CAF African Nations Championship
- Ratiba ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025 Hatua ya 16 Bora
Leave a Reply