Yanga SC Yazindua Jezi Mpya Ili Kulinda Mapato Dhidi ya Jezi Feki
Klabu ya Yanga SC imetangaza rasmi uzinduzi wa jezi mpya awamu ya pili ambazo zimeboreshwa kwa mabadiliko maalumu, hatua iliyochukuliwa ili kulinda mapato ya klabu dhidi ya wimbi la wauzaji wa jezi feki wanaoingiza sokoni bidhaa zisizo halali.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Meneja wa Habari wa Yanga SC, Ally Kamwe, alieleza kuwa baada ya awamu ya kwanza ya jezi kuhitimishwa, mwekezaji wa biashara hiyo alibaini uwepo wa idadi kubwa ya jezi feki zilizokuwa zikisambazwa sokoni. Hali hiyo ilionekana kuhatarisha mapato halisi ya klabu pamoja na kudanganya mashabiki wanaounga mkono timu kwa dhati.
Alama Maalumu Kutofautisha Jezi Halisi na Feki
Kwa mujibu wa Kamwe, jezi mpya za awamu ya pili zimeundwa kwa mfumo wa kipekee wenye alama mbili kuu za usalama zitakazomwezesha kila shabiki kutambua jezi halisi ya Yanga SC.
“Jezi hizi mpya zitakuwa na tofauti hapa kulia. Jezi za sasa zina logo ya mdhamini, lakini hizi mpya zitakuwa na neno NIA. Mashabiki watambue kuwa endapo wataona bado kuna jezi zenye logo ya GSM kuanzia sasa, hizo si halisi bali ni feki,” alisema Kamwe.
Alama nyingine iliyoongezwa ni maandishi ya 90N, ambayo yatakuwa yanaonekana wazi nje na ndani ya jezi. Tofauti na zile za awali, ambazo namba ya miaka ya Yanga (90) ilikuwa ikiandikwa juu lakini haikuonekana upande wa ndani, jezi mpya zinatoa uthibitisho wa wazi kwa shabiki anayeinunua.
Changamoto ya Biashara ya Jezi Feki
Kamwe alikiri kuwa biashara ya jezi imekumbwa na changamoto kubwa kutokana na uwepo wa watu wanaojihusisha na utengenezaji na uuzaji wa bidhaa feki.
“Ndugu zangu hii biashara ya jezi ina watu hatari sana. Tumejaribu kupambana nao kwa njia mbalimbali lakini bado changamoto ipo. Hata sasa, kuna makontena yenye jezi za msimu huu zilizopita zikisambazwa sokoni,” alisema Kamwe.
Kutokana na changamoto hiyo, klabu iliona ni vyema kuja na mkakati mpya wa uzinduzi wa jezi za kipekee ambazo zitaboresha mapato yake na kuondoa nafasi ya watu wasioitakia mema klabu kunufaika na kazi ya timu.
Mashabiki Wasisitize Kununua Jezi Halisi
Aidha, Kamwe alihimiza mashabiki wa Yanga SC kujitokeza kwa wingi kununua jezi mpya zilizozinduliwa. Tayari bidhaa hizo zimeanza kupatikana sokoni, na wapenzi wa klabu wanashauriwa kuzikimbilia ili kujihakikishia uhalisia wake na wakati huo huo kuchangia mapato ya klabu.
“Jezi mpya zimeshaingia sokoni. Tunawaomba mashabiki wetu wazikimbilie mapema ili kesho wapendeze uwanjani na kuonesha mshikamano na timu yao,” aliongeza.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
- Wafungaji Bora Ligi Kuu ya NBC Tanzania 2025/2026
- Uwanja wa Jamhuri Dodoma Kuwa Makazi Mapya ya Mtibwa Sugar
- Simba Yaanza Ligi Kuu 2025/26 Kwa Ushindi wa 3-0 Dhidi ya Fountain Gate
- Matokeo ya Simba vs Fountain Gate Leo 25/09/2025
- Ibenge Afungua Kampeni za Ligi Kuu kwa Ushindi wa 2-0 Dhidi ya Mbeya City
- Simba vs Fountain Gate Leo 25/09/2025 Saa Ngapi?
- Vilabu Bora Afrika 2025 (CAF Club Ranking 2025)
Leave a Reply