Xabi Alonso Atangazwa Kuwa Kocha Mpya wa Real Madrid Hadi 2028
Xabi Alonso ameteuliwa rasmi kuwa kocha mkuu wa Real Madrid, akitarajiwa kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti kuanzia msimu ujao wa 2025/26. Kocha huyo mwenye mafanikio makubwa akiwa na Bayer Leverkusen anajiandaa kuanzisha enzi mpya katika klabu hiyo ya kifalme ya Hispania. Mkataba wake wa miaka mitatu utaendelea hadi mwaka 2028, huku akiandaliwa kuanza kazi rasmi kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu yatakayofanyika nchini Marekani kati ya Juni 15 na Julai 13, 2025.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka kwa mchambuzi maarufu wa masuala ya uhamisho, Fabrizio Romano, Alonso ameafikiana na Real Madrid kusaini mkataba wa muda mrefu, akitarajiwa kuwasili Bernabeu pamoja na timu yake ya kiufundi, ikiwa ni pamoja na wasaidizi wake wa karibu. Ingawa Real Madrid haijatoa tamko rasmi hadi sasa, vyanzo vya karibu na klabu vinaeleza kuwa kila kitu kimekamilika na ni suala la muda tu kabla ya kutangazwa hadharani.
Kocha huyo wa zamani wa Bayer Leverkusen atachukua nafasi ya Carlo Ancelotti, ambaye amekuwa kwenye benchi la Real Madrid tangu mwaka 2021 katika awamu yake ya pili. Ancelotti, ambaye ameshinda mataji kadhaa ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili na La Liga mara mbili, anatazamiwa kujiunga na timu ya taifa ya Brazil baada ya kuhitimisha msimu huu na mechi tatu za mwisho za La Liga.
Safari ya Ukocha ya Xabi Alonso
Xabi Alonso si jina geni kwa mashabiki wa Real Madrid. Alicheza kama kiungo wa kati wa klabu hiyo kati ya mwaka 2009 hadi 2014, kipindi ambacho alijizolea heshima kutokana na uchezaji wake wa hali ya juu. Baada ya kustaafu soka, alianza kazi ya ukocha kwa kuinoa timu ya vijana ya Real Madrid yenye wachezaji chini ya miaka 14, kabla ya kupata nafasi katika kikosi cha pili cha Real Sociedad.
Mwaka 2022, Alonso alipewa jukumu la kuinoa Bayer Leverkusen ya Ujerumani, ambapo ameweka historia kwa kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Bundesliga bila kupoteza mechi hata moja. Aidha, ameshinda Kombe la Ujerumani pamoja na Super Cup ya Ujerumani, mafanikio yaliyomfanya kuwa mmoja wa makocha wanaoangaliwa kwa jicho la kipekee barani Ulaya.
Maandalizi ya Zama Mpya Madrid
Kutokana na mafanikio yake akiwa Leverkusen, Alonso amekuwa chaguo la kwanza kwa mabosi wa Real Madrid kuendeleza falsafa ya ushindi ya klabu hiyo. Klabu ina matumaini makubwa kwamba atasaidia kuunda kikosi cha ushindani kitakachojumuisha wachezaji chipukizi na mastaa waliopo kama Kylian Mbappe na Vinicius Jr.
Hata hivyo, Real Madrid pia inatarajia mabadiliko ya kizazi ndani ya kikosi, jambo linalompa Alonso jukumu zito la kuwaunganisha wachezaji wapya kama Endrick na Arda Guler na wale wa sasa katika mfumo mmoja wa ushindi. Katika hali ya nadra, viongozi wa Bayer Leverkusen wameonyesha uungwaji mkono kwa kocha wao kujiunga na Real Madrid. Wameeleza kuwa hatua hiyo ni kutimizwa kwa ndoto ya maisha ya Alonso na wamekubali kwa moyo mweupe kumpa nafasi hiyo muhimu katika taaluma yake ya ukocha.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Simba Sc vs KMC leo 11 May 2025 Saa Ngapi?
- Simba Yapewa Vitisho Vikali na KMC Kuelekea Mechi ya Kesho Mei 11, 2025
- Napoli Yajipanga Kumsajili Jack Grealish Kutoka Man City
- KENGOLD Yapanga Kuipeleka Simba Ruvuma Juni 18
- Simba SC Yakata Tiketi Ligi ya Mabingwa Afrika 2025-2026 Baada ya Kufikisha Pointi 66
- Yanga Yashikilia Msimamo wa Kutocheza Dabi Licha Ya Majibu ya CAS
- Simba Yaitandika JKT na Kujiweka Kwenye Njia ya Ligi ya Mabingwa
- Matokeo JKT Tanzania vs Simba Leo 05/05/2025
- Sababu 3 Zilizofanya CAS Kuitupilia Mbali Kesi ya Yanga
Leave a Reply