Nafasi Mpya za Kazi Serikalini 2025/2026 – Sekta ya Elimu, Afya, na Ulinzi Zapewa Kipaumbele

Nafasi Mpya za Kazi Serikalini 2025/2026 – Sekta ya Elimu, Afya, na Ulinzi Zapewa Kipaumbele

Serikali yatangaza nafasi mpya za kazi serikalini 2025/2026 zipatazo 41,500. Sekta za elimu, afya, na ulinzi zapewa kipaumbele huku utekelezaji wa ajira ukianza mara moja kupitia Ajira Portal.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi, ametangaza rasmi kuwa Serikali imetenga nafasi mpya za ajira 41,500 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayolenga kupunguza upungufu wa watumishi katika sekta muhimu nchini.

Akizungumza Oktoba 11, 2025 jijini Dodoma, Bw. Mkomi alisema kuwa sekta za elimu, afya, na ulinzi ndizo zimepewa kipaumbele katika mgao huu mpya wa ajira. Kati ya nafasi hizo, walimu watapatiwa ajira 12,176, sekta ya afya ngazi ya Serikali za Mitaa nafasi 10,280, na ajira 7,000 zimepangwa kwa taasisi za ulinzi ikiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji.

Sekta nyingine zitakazonufaika na ajira hizi ni kilimo (470 nafasi), mifugo (312 nafasi), uvuvi (47 nafasi) na kada nyinginezo (11,022 nafasi) ambazo zitagawanywa kulingana na mahitaji ya kila taasisi ya umma.

Nafasi Mpya za Kazi Serikalini 2025/2026 – Sekta ya Elimu, Afya, na Ulinzi Zapewa Kipaumbele

Utekelezaji wa Ajira Kuanzia Mwaka wa Fedha 2025/2026

Bw. Mkomi alibainisha kuwa utekelezaji wa ajira hizo utaanza mara moja, huku Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ikiendelea kukamilisha mchakato wa ajira zilizobaki za mwaka wa fedha 2024/2025.

“Ninaielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuanza mchakato wa kujaza nafasi hizo za mwaka 2025/2026, sambamba na kukamilisha nafasi zote zilizobaki za mwaka uliopita,” alisema Bw. Mkomi.

Kwa mujibu wa taarifa yake, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali ilitenga ajira 45,000, ambapo nafasi 30,863 tayari zimejazwa na wahusika kupangiwa vituo vya kazi, 6,701 zipo katika hatua ya upangaji, na 7,836 zinatarajiwa kukamilika kufikia mwezi Novemba 2025.

Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kufikia mwezi huo, vibali vyote vya ajira 86,500 vya miaka 2024/2025 na 2025/2026 vinakuwa vimekamilika na watumishi wote wapya wanaanza kazi rasmi.

Sekretarieti ya Ajira Yapewa Mamlaka Kamili

Katibu Mkuu alieleza kuwa Sekretarieti ya Ajira imepewa jukumu la kusimamia ajira zote za umma kwa kushirikiana na waajiri mbalimbali, wakiwemo TAMISEMI, Ofisi ya Msajili wa Hazina, na Wizara ya Afya.

“Waajiri wote wanapaswa kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti ya Ajira kuhakikisha zoezi la usaili linafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni,” alisema Bw. Mkomi.

Kwa mwaka huu wa fedha, usaili wa waombaji wa nafasi mpya za kazi serikalini 2025/2026 utafanyika katika kila mkoa wa Tanzania Bara na katika vituo maalum vya Zanzibar ili kupunguza gharama kwa waombaji na kurahisisha ushiriki wa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Barua za Ajira Kupatikana Kupitia Ajira Portal

Serikali imetangaza mabadiliko katika utoaji wa barua za ajira ili kupunguza usumbufu kwa waombaji. Bw. Mkomi alisema kuwa, kuanzia sasa, barua zote za ajira zitapatikana moja kwa moja kupitia akaunti za waombaji katika Ajira Portal.

“Hatutaki waombaji waje Dodoma kufuata barua. Barua zao za ajira zitawasilishwa kupitia akaunti zao za Ajira Portal,” alisema Bw. Mkomi.

Pia aliongeza kuwa waombaji watakaofaulu usaili lakini wasipangiwe kazi mara moja watahifadhiwa katika kanzidata (database) ya Sekretarieti ya Ajira, ili wapangiwe kazi pindi nafasi mpya zitakapotokea.

Kupunguza Upungufu wa Watumishi Serikalini

Bw. Mkomi alibainisha kuwa Serikali bado inakabiliwa na upungufu wa watumishi wa umma takribani 270,000, lakini jitihada zinaendelea kufanyika kupunguza pengo hilo kupitia utoaji wa ajira mpya kila mwaka.

Alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza ahadi yake ya kuajiri watumishi wapya kila mwaka, akisisitiza kuwa hatua hii inalenga kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, hususan katika sekta za elimu, afya, na ulinzi.

Uimarishaji wa Mifumo ya Kielektroniki Serikalini

Aidha, Bw. Mkomi alisema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya kusimamia utendaji kazi wa watumishi wa umma kupitia mifumo ya kielektroniki kama PEPMIS na PIPMIS.

“Ofisi itaendelea kuhakikisha mifumo ya kielektroniki inatumika kusimamia ajira, utendaji kazi na rasilimali watu ili kujenga utamaduni wa kuwajibika na kuongeza tija katika sekta ya umma,” alisema.

Mkomi alihitimisha kwa kuwataka watumishi wa umma kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, akisema kuwa ubora wa huduma ni kiashiria cha ufanisi wa Serikali na chachu ya kujenga taswira chanya kwa umma.

Tangazo hili la nafasi mpya za kazi serikalini 2025/2026 linatoa fursa kubwa kwa Watanzania wenye sifa kujiunga na ajira za umma katika sekta mbalimbali. Kwa kuzingatia kipaumbele katika elimu, afya, na ulinzi, Serikali inalenga kuimarisha utoaji wa huduma muhimu na kupunguza upungufu wa watumishi nchini.

Waombaji wanahimizwa kufuatilia taarifa rasmi kupitia mfumo wa Ajira Portal unaopatikana kupitia kiungo https://portal.ajira.go.tz/, ambako maelekezo, barua za ajira, na ratiba za usaili zitapatikana moja kwa moja bila usumbufu.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Majina ya Walioitwa Kwenye Usaili INEC 2025
  2. Mfumo wa Maombi ya Kazi Jeshi la Magereza 2025 | TPS Recruitment Portal
  3. Nafasi za Kazi Jeshi la Magereza 2025
  4. Mfano wa Barua ya Maombi ya Kazi Jeshi la Magereza
  5. Tangazo La Ajira Jeshi la Magereza 2025 Pdf
  6. Mwisho Wa Kutuma Maombi ya Ajira Jeshi la Magereza 2025
  7. Nafasi Mpya za Kazi MDAs & LGAs Juni 2025 – Tangazo la Ajira Serikalini Nafasi 6,732
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo