Fountain Gate vs Simba Leo 15/04/2026 Saa Ngapi?
Wekundu wa Msimbazi Simba SC leo watashuka dimbani kuwakabili wenyeji wao Fountain Gate FC katika mchezo wa ligi kuu ya NBC ambao utatimua vumbi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha saa 4:00 pm. Mchezo huo unatarajiwa kuvuta hisia nyingi kutokana na umuhimu wake kwa pande zote mbili, huku kila timu ikiingia uwanjani ikihitaji pointi tatu.
Mtihani wa kwanza kwa Minziro dhidi ya Simba
BAADA ya kukabidhiwa majukumu ya kuiongoza Fountain Gate, Fred Felix ‘Minziro’ na benchi lake la ufundi wanatarajia kuanza kazi kwa mechi ngumu dhidi ya Simba. Minziro na msaidizi wake, Mathias Wandiba, walitambulishwa kikosini Aprili 10, 2026, wakichukua nafasi ya Mohamed Ismail ‘Laizer’.
Kocha huyo mwenye uzoefu tayari alikuwepo jukwaani alipoishuhudia Fountain Gate ikipokea kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya Azam katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 16 bora. Simba, kwa upande mwingine, iliitandika Dodoma Jiji mabao 3-1 na kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopo, Fountain Gate itakuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Kila timu inaingia uwanjani ikiwa na lengo la kupata ushindi ili kujipatia nafasi nzuri kwenye msimamo.
Hali ya timu kabla ya mchezo
Hadi sasa, Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 36, na inaachwa pointi nane na Yanga waliopo kileleni. Fountain Gate inashika nafasi ya 14 kwa pointi 16 baada ya timu zote kucheza mechi 17.
Minziro alitua Fountain Gate akitokea Bigman FC ya Ligi ya Championship. Kabla ya hapo, ameshazifundisha timu kadhaa kwa mafanikio, zikiwemo KMC, Geita Gold na Singida Big Stars alizozipandisha Ligi Kuu. Pia aliwahi kuitumikia Mbao FC nusu msimu kabla ya kushuka nayo daraja.
Meneja wa Fountain Gate, Elias Zamkufo, alisema wanatambua ugumu wa mchezo huo, lakini wanaamini uzoefu wa benchi la ufundi unaweza kusaidia timu kupata ushindi na kujinasua kwenye nafasi za chini. Alisema wachezaji wote wako fiti na waliokuwa majeruhi Daniel Joram na Ibrahim Parapanda wamerejea.
Zamkufo alisema: “Tunajua Simba ni timu kubwa na ukifanya makosa wanakuadhibu, hatupaswi kumdhibiti mchezaji mmoja bali kuwakabili wote, tunashukuru Kocha wetu anao uzoefu na ushindani kwenye soka.
“Mbinu zake zinaweza kutupa kitu, kimsingi tuko tayari kwa ajili ya mchezo huo ili kupata pointi tatu ambazo zitatupandisha nafasi nzuri kwenye msimamo, mashabiki waje kwa wingi kutusapoti.”
Mapendekezo ya Mhariri:







Leave a Reply