Cv ya Allan Okello Kiungo Mpya wa Yanga Sc 2025/2026
Klabu ya Wananchi, Young Africans SC (Yanga), imemtambulisha rasmi kiungo mshambuliaji kutoka Uganda, Allan Okello, kama usajili mpya kwa msimu wa 2025/2026. Usajili huo ulithibitishwa jijini Dar es Salaam Januari 12, 2026, baada ya Yanga kukamilisha dili na klabu ya Vipers, hatua iliyovuta hisia za wadau wa soka kutokana na hadhi na rekodi za mchezaji huyo.
Wasifu Kamili (CV) ya Allan Okello
Kulingana na wasifu wa mchezaji huyo, Allan Okello alizaliwa tarehe 04 Julai 2000 mjini Lira, Uganda, na ana umri wa miaka 25. Ana urefu wa mita 1.79, ni raia wa Uganda, na anatumia zaidi mguu wa kushoto. Nafasi yake kuu ni kiungo mshambuliaji, ingawa ana uwezo wa kucheza pia kama winga wa kushoto au kulia kulingana na mahitaji ya timu.
Okello ni mchezaji wa Young Africans SC, alijiunga na klabu hiyo tarehe 10 Januari 2026, huku mkataba wake ukiwa na muda wa hadi tarehe 31 Desemba 2028. Anasimamiwa na wakala wa wachezaji wa NextPro Sports.
Gharama ya Usajili na Rekodi ya Vipers
Yanga ilikamilisha usajili wa Okello kwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 300,000, sawa na takribani Shilingi milioni 740. Ada hiyo imeiwezesha klabu ya Vipers kuvunja rekodi ya mauzo ya wachezaji wake, na kumfanya Okello kuwa mchezaji wa pili ghali zaidi kuwahi kuuzwa na klabu hiyo, nyuma ya Farouk Miya pekee.
Dili hilo lilikamilika baada ya mazungumzo ya pande zote kati ya uongozi wa Yanga na Vipers, yaliyohitimishwa jijini Kampala, Uganda.
Ubora wa Kiufundi na Takwimu
Takwimu za uchezaji wa Allan Okello zinaonesha mchezaji mwenye mchango mkubwa katika safu ya ushambuliaji. Akiwa na Vipers katika Ligi Kuu ya Uganda msimu wa sasa, alihusika katika mabao matano ndani ya mechi saba, akifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mwisho.
Msimu uliotangulia, Okello alihusika moja kwa moja katika mabao 23 ya Vipers, akifunga mabao 19 na kutoa pasi tatu za mabao, mafanikio yaliyomuweka kileleni kama Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Uganda. Ufanisi huo unaonesha uwezo wake wa kufunga na kusoma mchezo katika eneo la mwisho la uwanja.
Uzoefu wa Kimataifa
Mbali na mafanikio ya klabu, Okello ana uzoefu katika mashindano ya kimataifa baada ya kuichezea Vipers na KCCA FC katika michuano ya Afrika. Vilevile, ameitumikia timu ya taifa ya Uganda katika mechi 36, akifunga mabao sita na kutoa pasi 10 za mwisho, takwimu zinazoonesha mchango wake wa moja kwa moja katika mafanikio ya timu ya taifa.
Nidhamu Ndani ya Uwanja
Moja ya sifa zinazomtofautisha Allan Okello ni nidhamu yake ya hali ya juu. Akiwa na timu ya taifa ya Uganda, hajawahi kuonyeshwa kadi yoyote. Katika ngazi ya klabu, hajawahi kupewa kadi nyekundu, na ameonyeshwa kadi za njano tatu pekee tangu aanze kucheza soka la ushindani, hali inayoashiria umakini na uchezaji wa kitaaluma.
Kutokuwepo Ligi ya Mabingwa Afrika Msimu Huu
Kwa msimu wa 2025/2026, Yanga haitamtegemea Okello katika michuano ya kimataifa ya Afrika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tayari alishacheza Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Vipers katika msimu huu, jambo linalomfanya kukosa sifa ya kushiriki mashindano hayo na Yanga hadi msimu ujao.
Okello amewahi kucheza nje ya Uganda alipokuwa na klabu ya Paradou AC ya Algeria kwa kipindi cha miaka miwili. Hata hivyo, alirejea nyumbani baada ya kushindwa kuhimili mazingira ya soka la huko. Kwa upande wa Tanzania, mazingira na hali ya hewa ya Afrika Mashariki yanatajwa kuwa rafiki zaidi kwake, jambo linalotarajiwa kumsaidia kuonyesha kiwango chake halisi akiwa na Yanga.
Mapendekezo ya Mhariri:









Leave a Reply