Cv ya Mohammed Bajaber Kiungo Mshambuliaji Mpya Simba Sc 2025/2026
Klabu ya Simba SC imemtambulisha kiungo mshambuliaji mpya, Mohammed Bajaber, raia wa Kenya mwenye umri wa miaka 22, kama sehemu ya usajili wao kuelekea msimu wa mashindano wa 2025/2026. Ujio wa Bajaber, aliyejizolea umaarufu mkubwa ndani ya muda mfupi kwenye soka la Afrika Mashariki, unaashiria dhamira ya klabu hiyo kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji kuelekea kampeni ya Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa ya CAF.
Wasifu wa Mohammed Bajaber
Mohammed Bajaber alizaliwa mwaka 2003 nchini Kenya na ni zao la akademia ya Starfield. Akiwa kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kucheza kama winga wa kushoto, wa kulia, na pia namba 10, amejijengea jina kama mchezaji mwenye kasi, ubunifu na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao.
Bajaber alianza msimu wa 2024/2025 akiwa na Nairobi City Stars, kabla ya kutua Kenya Police FC mwanzoni mwa mwaka 2025 kwa dau la Ksh 1 milioni. Katika muda mfupi ndani ya kikosi hicho, alijidhihirisha kama moja ya wachezaji bora zaidi wa ligi, akiisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Takwimu Muhimu za Uchezaji
Katika msimu wake wa mwisho na Kenya Police, Bajaber alifunga mabao 11 na kuchangia kupatikana kwa mabao manne zaidi. Ufanisi huo ulimfanya kuwa mmoja wa wachezaji wa kutegemewa kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, na hatimaye kuvutia macho ya Simba SC.
Uzoefu wa Kimataifa
Mbali na mafanikio ya ndani, Bajaber aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, chini ya kocha Benni McCarthy. Katika mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Gambia, Bajaber aliingia kama mchezaji wa akiba na kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju mzuri, jambo lililomletea sifa kutoka kwa wadau wa soka. Ingawa alikumbwa na majeraha ya msuli wa paja daraja la pili, bado aliitwa kwenye kikosi cha CHAN 2024, kabla ya kuondolewa kambini ili kukamilisha uhamisho wake kwenda Simba.
Mkataba na Simba SC
Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizopo, Bajaber amesaini mkataba wa miaka mitatu na Simba SC. Chanzo cha habari kutoka Kenya kimeeleza kuwa Kenya Police FC ilipokea kiasi cha Ksh 12.9 milioni sawa na dola 100,000, na hivyo kupata faida kubwa ukizingatia waliwanunua mchezaji huyo kutoka Nairobi City Stars kwa Ksh 1 milioni pekee.
Bajaber anatarajiwa kuungana na kikosi cha Simba kilichoko kambini nchini Misri kwa maandalizi ya msimu mpya. Atakuwa chini ya Kocha Mkuu Fadlu David, ambapo ataanza kujiweka sawa kushiriki mechi za kirafiki na michuano ya ndani pamoja na ile ya Afrika.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Picha za Wachezaji Wapya wa Simba 2025/2026
- Pamba Jiji FC Yamtambulisha Francis Baraza Kama Kocha Mkuu 2025/2026
- CV ya Alassane Kante Kiungo Mpya Simba 2025/2026
- CV Ya Rushine De Reuck Beki Mpya wa Simba 2025/2026
- Simba SC Yasaini Mkataba wa Sh20 Bilioni na Betway Kama Mdhamini Mkuu
- Wachezaji Wapya wa Yanga 2025/2026
- CV ya Moussa Balla Conte Mchezaji Mpya wa Yanga Sc 2025/2026
Leave a Reply