HESLB Yatangaza Kufunguliwa kwa Dirisha la Maombi ya Mikopo 2025/2026

HESLB Yatangaza Kufunguliwa kwa Dirisha la Maombi ya Mikopo 2025/2026

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) yafungua rasmi Dirisha la Maombi ya Mikopo 2025/2026, huku kiasi cha Shilingi bilioni 917 kikiwa kimetengwa kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa wanafunzi watakaokidhi vigezo. Mwongozo wa jinsi ya kuomba, pamoja na masharti muhimu, umetolewa ili kuwaongoza waombaji katika hatua zote za mchakato huu wa kidijitali.

Katika taarifa iliyotolewa rasmi jijini Dar es Salaam mnamo Juni 19, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alithibitisha kuwa jumla ya Shilingi bilioni 916.7 zimetengwa kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Fedha hizo zinatarajiwa kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 99,620 wa mwaka wa kwanza katika ngazi mbalimbali za elimu, ikiwa ni pamoja na:

  • Diploma (Stashahada)
  • Shahada ya Kwanza (Degree)
  • Shahada za Uzamili (Postgraduate)

Kwa upande wa shahada ya kwanza pekee, wanafunzi 88,000 watapata mikopo, ikiwa ni ongezeko la 8,000 kutoka wanafunzi 80,000 waliopata mikopo katika mwaka uliopita wa 2024/2025.

Aidha, kwa mwaka huu wa masomo, wanafunzi 10,000 wa stashahada pia wamenufaika na mpango huo, ikilinganishwa na 7,000 wa mwaka jana ongezeko kubwa la wanafunzi 3,000 zaidi.

HESLB Yatangaza Kufunguliwa kwa Dirisha la Maombi ya Mikopo 2025/2026
HESLB Yatangaza Kufunguliwa kwa Dirisha la Maombi ya Mikopo 2025/2026

Fedha za Mikopo Kuendelea Kufaidisha Wanafunzi Walioko Vyuo

Mbali na wanafunzi wapya, kiasi hicho cha fedha pia kitagharimia mahitaji ya wanafunzi 173,783 wanaoendelea na masomo yao katika vyuo mbalimbali hapa nchini. Dkt. Kiwia alieleza kuwa hatua hii inalenga kuendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa wote bila kujali hali ya kiuchumi ya familia zao.

“Tunaendelea kupanua wigo wa walionufaika na mikopo ya elimu ya juu. Hata kwa wanafunzi wa diploma, idadi yao inaongezeka mwaka huu. Lengo letu ni kutoa nafasi sawa kwa kila kijana mwenye sifa ya kuendelea na elimu ya juu,” alisema Dkt. Kiwia.

Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Kassim Ndumbo, alisema kuwa hatua ya HESLB kufadhili wanafunzi wa vyuo vya kati inawapa matumaini wengi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kifedha.

“Tulikuwa tunashuhudia vijana wengi wakiachana na masomo kwa sababu ya kushindwa kumudu ada. Kupitia mikopo hii, ndoto zao sasa zinaanza kutimia,” alisema Ndumbo.

TASAF na HESLB Washirikiana Kufanikisha Mikopo kwa Kaya Maskini

Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Godwin Mkisi, alithibitisha kuwa zaidi ya wanafunzi 11,000 kutoka kaya masikini wamepata mikopo kwa kiwango cha asilimia 100 kupitia ushirikiano wa TASAF na HESLB.

“Tunafahamu kuwa mikopo hutolewa kulingana na hali ya mwanafunzi, lakini kwa upande wa wanaotoka katika mazingira magumu zaidi, tumewahakikishia mikopo ya asilimia 100,” alisema Mkisi.

Dirisha la Maombi ya Mikopo 2025/2026 Lafunguliwa Rasmi – Juni 15 hadi Agosti 31, 2025

HESLB imetangaza kuwa dirisha rasmi la uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026 lilifunguliwa tarehe 15 Juni, 2025 na linatarajiwa kufungwa tarehe 31 Agosti, 2025.

Kwa wanafunzi wa stashahada (Diploma) wanaotarajia kuanza masomo mwezi Machi 2026, dirisha la maombi litafunguliwa tena tarehe 1 Februari hadi 31 Machi, 2026.

Muda wa Maombi:

  • 📅 15 Juni – 31 Agosti 2025 (Kwa wanaoanza masomo Septemba)
  • 📅 1 Februari – 31 Machi 2026 (Kwa wanaoanza masomo Machi)

Maelekezo Muhimu kwa Waombaji WA Mikopo

Dkt. Kiwia alisisitiza kwamba waombaji wote wanatakiwa kusoma Mwongozo wa Uombaji Mkopo kupitia tovuti rasmi ya HESLB (www.heslb.go.tz) kabla ya kuanza mchakato wa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mfumo wa kidijitali wa OLAMS.

Vitu Muhimu vya Kuzingatia:

  • Anwani za makazi (NaPA): Waombaji wanatakiwa kuweka namba ya barua ya utambulisho ya NaPA katika mfumo wa maombi.
  • Akaunti ya Benki: Kila mwombaji anatakiwa kuwa na akaunti ya benki yenye jina linalolingana na jina kwenye cheti cha kidato cha nne
  • Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN): Ikiwepo, ijazwe. Kama huna, unaweza kuendelea na maombi.

Samia Scholarship: Nafasi kwa Waliofaulu Sayansi

Kwa mwaka wa masomo 2025/2026, ufadhili wa Samia Scholarship utatolewa kwa wanafunzi 700 waliopata ufaulu wa juu kwenye tahsusi za sayansi katika mtihani wa kidato cha sita ulioendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Matokeo ya Kidato cha Sita 2025 NECTA ACSEE
  2. Matokeo ya Kidato cha Sita 2025 (NECTA Form Six Results)
  3. Tarehe ya Kutangazwa kwa Matokeo ya Kidato cha Sita 2025 na NECTA
  4. Fomu Za Kujiunga Kidato Cha Tano (Form Five Joining Instruction Form) 2025
  5. Majina ya Waliochaguliwa Kidato cha Tano 2025/2026 (Form Five Selection)
  6. Shule Walizopangiwa Kidato cha Tano Zanzibar 2025
  7. Majina ya Waliochaguliwa Vyuo Vya Kati 2025/2026 (Selection Vyuo Vya Kati)
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo