Fountain Gate Yazindua Dimba la Tanzanite Kwaraa kwa Ushindi Ligi Kuu
Timu ya Fountain Gate imetoa ishara ya kujiimarisha katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Ken Gold. Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, ilivuta hisia za mashabiki wengi wa soka, hasa kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kwa mkoa wa Manyara kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu tangu kugawanywa kutoka Arusha mwaka 2002.
Fountain Gate ilipata ushindi wake wa pili mfululizo katika msimu huu, huku mechi hii ikileta furaha kwa wakazi wa mji wa Babati na maeneo jirani kama Bonga, Kona Nakwa, Sigino, Kiru, Sawe, Oysterbay, na Singe. Ushindi huo umekuwa ni zawadi maalum kwa wapenzi wa soka mkoani Manyara ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikosa fursa ya kushuhudia mpambano wa aina hii.
Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote mbili zikijaribu kusaka bao la mapema. Ken Gold, timu inayoshiriki kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu, ilifanikiwa kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 9 kupitia mchezaji Joshua Ibrahim, aliyeunganisha pasi maridadi kutoka kwa nahodha Mishamo Daud. Bao hilo liliwatuliza Ken Gold kwa muda, lakini Fountain Gate haikuchoka kulisakama lango la wapinzani wao.
Dakika ya 42, juhudi za Fountain Gate ziliwalipa baada ya mpira wa pili uliopanguliwa na kipa wa Ken Gold kumkuta AbalKassim Suleiman, ambaye alitumia nafasi hiyo vyema na kusawazisha bao. Hatua hiyo ilileta msisimko zaidi kwa mashabiki wa Fountain Gate na wapenzi wa soka waliokuwa wakishuhudia mechi hiyo.
Bao la Ushindi
Fountain Gate haikuishia hapo, kwani katika dakika ya 57 Selemani Mwalimu alifunga bao la pili na la ushindi, akipeleka shangwe na nderemo kwa wakazi wa Babati na maeneo mengine ya mji huo. Bao hilo lilifungwa kutokana na mpira wa kurusha uliochezwa haraka, ambapo Mwalimu alimalizia kwa ustadi mkubwa.
Msimamo wa Timu
Ushindi huo umeifanya Fountain Gate kufikisha pointi sita baada ya michezo mitatu, ambapo imepata ushindi mara mbili na kupoteza mara moja. Timu hiyo sasa inajivunia mabao manne huku ikifungwa mabao matano. Hali hii inaashiria kuwa Fountain Gate iko katika nafasi nzuri ya kuendelea kupanda juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Ken Gold, timu hiyo imeendelea kuchemka kwenye michezo yake ya mwanzo ya Ligi Kuu. Huu ulikuwa mchezo wao wa pili kupoteza mfululizo, baada ya awali kufungwa 3-1 na Singida Black Stars. Ken Gold inaonekana bado inahitaji muda wa kuzoea mazingira ya Ligi Kuu kutokana na ukweli kwamba wanashiriki kwa mara ya kwanza msimu huu.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti