Gamondi Atamba na Singida BS Baada ya Kutwaa Ubingwa wa Haraka

Gamondi Atamba na Singida BS Baada ya Kutwaa Ubingwa wa Haraka

Kocha mpya wa Singida Black Stars (Singida BS), Miguel Gamondi, ameandika historia ya kipekee baada ya kuiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa kwanza ndani ya mwezi mmoja tangu kuteuliwa. Akizungumza kwa furaha, Gamondi alisema ushindi huo ni mwanzo mzuri wa safari yake Singida BS na uthibitisho wa mradi mkubwa wa kujenga kikosi imara kitakachoshindana ndani na nje ya Tanzania.

“Kwa kweli najisikia fahari kubwa. Nilipozungumza kwa mara ya kwanza na uongozi, walinionyesha imani kubwa kwangu, na sasa tumelipa imani hiyo kwa kuwaletea taji la kwanza katika historia ya klabu hii,” alisema Gamondi, ambaye pia alitwaa tuzo ya Kocha Bora wa michuano ya 47 ya Cecafa Kagame Cup iliyofanyika Septemba 2-15.

Gamondi Atamba na Singida BS Baada ya Kutwaa Ubingwa wa Haraka

Safari ya Ubingwa wa Singida BS Chini ya Gamond

Katika mchezo wa fainali uliochezwa dhidi ya Al Hilal ya Sudan, Singida BS walionyesha ubora mkubwa licha ya kukutana na wapinzani wenye uzoefu wa kimataifa. Gamondi alikiri haikuwa kazi rahisi, lakini alisifu ari na mshikamano wa wachezaji wake ambao walipambana hadi dakika ya mwisho.

“Hakukuwa na kitu rahisi. Tulicheza na timu yenye historia kubwa, lakini vijana wangu walionyesha ari ya ajabu na kiwango bora cha ushindani, kana kwamba ni mechi ya Ligi ya Mabingwa. Hilo linanifanya niamini tunajenga kitu kikubwa hapa,” alisema kocha huyo.

Kwa mtindo wa kushambulia aliouanzisha, Singida BS walifunga mabao manne kwenye michezo miwili muhimu nusu fainali dhidi ya KMC (2-0) na fainali dhidi ya Al Hilal (2-1). Hii ni ishara kuwa falsafa yake ya soka la kushambulia inaanza kueleweka na kuzaa matunda.

Nyota Waliomkosha Gamondi

Miongoni mwa wachezaji walioibuka na kung’ara ni Clatous Chama, kiungo mshambuliaji wa kimataifa kutoka Zambia. Gamondi alisema hakushangazwa na kiwango chake kwani anamfahamu kwa muda mrefu na alijua uwezo wake wa kufanya maamuzi magumu uwanjani.

“Wengi walishangazwa na Chama, lakini mimi sikushangaa hata kidogo. Ni mchezaji mkubwa, na umri kwake si tatizo. Kwa kweli ni rahisi zaidi kufanya kazi na mchezaji mwenye akili kubwa ya mpira kama yeye,” aliongeza.

Pia aliwataja Khalid Aucho (nahodha wa timu) na Morice Chukwu kuwa miongoni mwa wachezaji wenye “ADN ya ushindi”, wakitoa uthibitisho kuwa Singida BS sasa imejipanga kwa malengo makubwa.

Maandalizi kwa Mashindano Makubwa Zaidi

Gamondi alisema ubingwa wa Kagame Cup unakuwa chachu ya maandalizi kwa safari mbili muhimu zinazowakabili: Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/26 na Kombe la Shirikisho la CAF.

“Ni bora kuendelea kujifunza kwa mtindo wa ushindi. Tukishinda, tunajenga hali ya kujiamini na mshikamano mkubwa zaidi. Hii ni hatua sahihi kuelekea changamoto kubwa zijazo,” alisema kocha huyo.

Singida BS inatarajiwa kuanza kampeni ya kimataifa kwa kuvaana na Rayon Sports ya Rwanda kwenye mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho kabla ya kurejea nchini kwa Ligi Kuu.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Ratiba ya Mechi za Leo 18 September 2025
  2. Simba SC Yaondoka na Kikosi cha Wachezaji 23 kuelekea Botswana Leo 17/09/2025
  3. Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
  4. CAF Yaipiga Simba Faini ya Dola 50,000 na Marufuku ya Mashabiki
  5. Chama Aipa Singida Bs Ubingwa Wa CECAFA Kagame Cup 2025
  6. Bao la Dakika za Jioni Dhidi ya Burnley Lairudisha Liverpool kileleni EPL
  7. Man City Yaibuka na Ushindi wa 3-0 Dhidi ya Manchester United
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo