JKU FC Mabingwa Wa Ngao ya Jamii Zanzibar 2024
Klabu ya JKU FC imeendelea kuandika historia kwenye soka la Zanzibar baada ya kutwaa tena taji la Ngao ya Jamii kwa mwaka 2024. Katika mchezo uliopigwa jioni ya Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja, JKU ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chipukizi, timu iliyowahi kuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho Zanzibar (ZFF). Ushindi huu unaashiria mwanzo mzuri wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zanzibar 2024-2025.
Safari ya Ushindi wa JKU FC
JKU FC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na ari ya kuendeleza ubabe wao katika soka la visiwani. Msimu uliopita, JKU ilitwaa taji hili baada ya kuifunga KMKM kwa mabao 5-2. Mwaka huu, Chipukizi waliingia na nia ya kulipa kisasi, lakini walishindwa kuhimili kasi ya JKU, ambao walijipatia mabao ya kila kipindi na kuondoka na ushindi wa 2-0.
JKU FC walifungua ukurasa wa mabao dakika ya 9 kupitia kwa mchezaji wao nyota, Ahmed Khamis. Bao hilo la mapema liliwapa JKU udhibiti wa mchezo na kuwafanya Chipukizi kutafuta usawa bila mafanikio. Licha ya juhudi za Chipukizi za kusawazisha, JKU walionekana kuwa na umakini mkubwa katika safu yao ya ulinzi, huku wakiweka presha kwa wapinzani wao kwa mashambulizi ya kushitukiza.
Katika kipindi cha pili, timu zote mbili zilifanya mabadiliko ya wachezaji, lakini JKU ndio walionekana kuwa na lengo la kumaliza mchezo mapema. Dakika ya 82, Koffi Hamza alihakikisha ushindi kwa JKU baada ya kufunga bao la pili ambalo lilikuwa ni kama msumari wa mwisho kwenye jitihada za Chipukizi kujaribu kurudi mchezoni. Bao hili lilihitimisha ndoto za Chipukizi za kushinda taji hilo.
Changamoto za JKU Katika Michuano ya Kimataifa
Licha ya mafanikio haya ya ndani, JKU FC inakabiliwa na changamoto katika michuano ya kimataifa. Timu hiyo ilitolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 9-1. Katika mechi hizo, JKU ilipoteza kwa mabao 6-0 na 3-1, mechi zote zikichezwa jijini Cairo baada ya maafande hao kukubaliana kucheza mechi zote ugenini kwa ombi la wapinzani wao.
Mechi hii ya Ngao ya Jamii ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kwa mwaka 2024-2025. Msimu huu unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na ushiriki wa timu 16, zikiwemo timu nne mpya zilizopanda daraja.
Timu hizo ni Muembe Makumbi City, Inter Zanzibar, Junguni, na Tekeleza, ambazo zimechukua nafasi ya timu zilizoshuka daraja, yaani Ngome, Kundemba, Jamhuri, na Maendeleo.
JKU FC inajiandaa kwa msimu mwingine wenye changamoto, ikiwa na lengo la kutetea taji la Ligi Kuu Zanzibar baada ya kulibeba msimu uliopita kwa kufikisha pointi 66, na hivyo kuiondoa KMKM kwenye utawala wa misimu mitatu mfululizo.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti