Kaizer Chiefs Ya Thibitisha Kuachana na Kocha Nasreddine Nabi

Kaizer Chiefs Ya Thibitisha Kuachana na Kocha Nasreddine Nabi

Klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imethibitisha rasmi kuachana na kocha wao mkuu, Nasreddine Nabi, kwa makubaliano ya pande zote mbili, hatua inayoashiria mwisho wa ushirikiano ulioanza mwezi Julai mwaka 2024. Hivyo, kocha huyo raia wa Tunisia na aliyewahi kuinoa Young Africans SC ya Tanzania sasa yupo huru kujiunga na timu yoyote atakayochagua.

Kupitia taarifa iliyotolewa na uongozi wa Amakhosi, pande hizo mbili zilifikia makubaliano hayo baada ya mazungumzo ya kujenga na yenye heshima. Uongozi wa klabu ulisisitiza kuwa maamuzi hayo yamefanyika “kwa misingi ya heshima na uelewano wa pande zote,” wakitoa shukrani kwa mchango wa Nabi katika kipindi chote cha kazi yake klabuni hapo.

“Kaizer Chiefs FC na kocha mkuu Nasreddine Nabi wanathibitisha kuwa baada ya mazungumzo mazuri, wamekubaliana kumaliza rasmi uhusiano wao wa kikazi kwa njia ya amani. Pande zote mbili zinatambua umuhimu wa maamuzi haya kuwasilishwa kwa heshima na mtazamo chanya, yakionesha uhusiano wa kiungwana uliodumu wakati wote wa ajira,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

Kaizer Chiefs Ya Thibitisha Kuachana na Kocha Nasreddine Nabi

Historia Fupi ya Ushirikiano Kati ya Nabi na Kaizer Chiefs

Kocha Nasreddine Nabi alijiunga na Kaizer Chiefs mwanzoni mwa msimu uliopita akiwa na matumaini makubwa ya kurejesha makali ya klabu hiyo yenye historia ndefu katika soka la Afrika Kusini. Ujio wake ulipokewa kwa matumaini makubwa na mashabiki wa Amakhosi, wakiamini ataweza kuleta mabadiliko kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa na Young Africans.

Hata hivyo, safari ya Nabi haikuwa rahisi. Klabu ilikumbwa na changamoto za kupata matokeo ya kuridhisha, hali iliyosababisha Chiefs kumaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita. Licha ya changamoto hizo, kocha huyo mwenye uzoefu alifanikiwa kufuta kiu ya mashabiki baada ya kuipa Chiefs ubingwa wa Kombe la Nedbank 2025, kwa ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya Orlando Pirates katika fainali iliyopigwa mwezi Mei.

Sababu za Kuachana

Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaonyesha kuwa uhusiano kati ya Nabi na uongozi wa Kaizer Chiefs ulianza kuyumba wiki chache zilizopita, baada ya timu kupoteza kwa mabao 3–1 dhidi ya Sekhukhune United katika mchezo wa Ligi ya Betway Premiership uliofanyika kwenye Uwanja wa FNB.
Baada ya kipigo hicho, kocha huyo alionekana kutoshiriki kwenye shughuli za klabu, hatua iliyozua maswali kuhusu mustakabali wake. Ripoti zinaeleza kuwa kulikuwa na “hitilafu ya uaminifu” baina ya pande hizo mbili, hali iliyochangia kufikia uamuzi wa kumaliza ushirikiano wao.

Ujumbe wa Shukrani

Kupitia ujumbe wake wa kuaga, Nasreddine Nabi alitoa shukrani kwa uongozi wa Kaizer Chiefs, wafanyakazi, wachezaji na mashabiki kwa ushirikiano na sapoti waliompa wakati wote alipokuwa klabuni hapo.

“Kocha Nabi anatoa shukrani zake za dhati kwa Kaizer Chiefs FC, viongozi wake, wafanyakazi, wachezaji na mashabiki kwa kujitolea na kumuunga mkono katika kipindi chote cha kazi yake,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, klabu ilimpongeza Nabi kwa mafanikio aliyoyapata, ikiwemo kuiongoza timu kutwaa taji la kihistoria la Nedbank Cup, na kumtakia kila la heri katika safari yake ya baadaye ya ukocha.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Matokeo Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars vs Zambia Leo Oktoba 8 2025
  2. Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
  3. Msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar PBZ 2025/2026
  4. Tanzania vs Zambia Leo Oktoba 8 2025 Saa Ngapi?
  5. FIFA Yairuhusu Fountain Gate Kufanya Usajili Nje ya Dirisha la Usajili
  6. FIFA Yamteua Eng. Hersi Said Kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Vilabu ya Wanaume Duniani
  7. Djigui Diarra Ashinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Septemba 2025/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo