KMKM Mabingwa wa FA Cup Zanzibar 2025 Baada ya Ushindi wa 4-2
Timu ya KMKM imetwaa rasmi ubingwa wa FA Cup Zanzibar 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Chipukizi, katika mchezo wa fainali uliopigwa Juni 21, 2025, kwenye Uwanja wa Mao Zedong, uliopo Mjini Unguja.
Ushindi huu wa kishindo umeweka historia mpya kwa KMKM, huku ukiwanyima Chipukizi fursa ya kutetea taji lao na kuiwakilisha Zanzibar kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Mchezo huo ulianza saa 1:00 usiku kwa hali ya ushindani mkubwa, huku kila timu ikihitaji kutwaa ubingwa. KMKM walionyesha dhamira ya ushindi mapema, wakiongozwa na mchezaji wao mahiri Jasper Yaw ambaye aliipatia timu yake bao la kwanza dakika ya 15 ya mchezo. Bao hilo liliongeza presha kwa Chipukizi, na hali hiyo ikaendelea kuwa ngumu zaidi dakika chache baadaye, Haji Makame alipoongeza bao la pili kwa KMKM.
Chipukizi, ambao walikuwa wakitetea taji hilo, walifanikiwa kurejesha matumaini kupitia bao la Faki Mwalimu katika dakika ya 38. Hata hivyo, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa KMKM wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ile ile, KMKM wakiendeleza mashambulizi ya kusisimua. Haji Makame kwa mara nyingine alionesha uwezo wake mkubwa kwa kufunga bao la tatu kwa KMKM, akizidi kuzamisha matumaini ya Chipukizi. Hatimaye, Abraham Othman alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga goli la nne, ambalo lilionekana kuzima kabisa juhudi za wapinzani wao.
Chipukizi walipata bao la pili kupitia Abdallah Nassor dakika ya 89, lakini ilikuwa ni pole kwao kwani muda ulikuwa umeisha na mchezo ukamalizika kwa KMKM kushinda mabao 4-2.
Kupitia ushindi huu wa kihistoria, KMKM sasa wataiwakilisha Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao. Hii ni nafasi adhimu kwa mabingwa hao wapya wa FA Cup Zanzibar 2025 kuonesha uwezo wao katika anga za kimataifa.
Wakati huo huo, timu ya Mlandege, ambao walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Klabu ya Liverpool Yamwaga Mamilioni Kumnasa Florian Wirtz
- Viingilio Simba SC vs Kagera Sugar 22/06/2025
- Viingilio Yanga VS Dodoma Jiji 22/06/2025
- Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
- Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
- Kaizer Chiefs Wavamia Dili la Yanga SC Kunasa Saini ya Percy Tau
- Mashujaa FC Yaanza Harakati za Kumsajili Beki wa Simba SC
Leave a Reply