Azam FC Yavunja Ukame wa Ushindi Ugenini Kwa Kuichapa Dodoma Jiji 3-0

Azam FC Yavunja Ukame wa Ushindi Ugenini Kwa Kuichapa Dodoma Jiji 3-0

Wana Rambaramba wa Chamanzi Azam FC hatimaye wamevunja ukame wa ushindi katika mechi za ugenini baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Machi 11, 2026 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Ushindi huo umefika baada ya Azam FC kucheza mechi mbili za ugenini kwa dakika 180 bila kupata ushindi, ikikusanya pointi mbili pekee kabla ya kurejea na ushindi huo mnono dhidi ya Dodoma Jiji.

Mchezo huo ulianza saa 1:15 usiku katika uwanja uliokuwa na hali ngumu ya kuchezea kutokana na mvua iliyonyesha kabla ya mechi, hali iliyosababisha sehemu nyingi za uwanja kuwa na tope lililochanganyika na maji.

Azam FC ilianza kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao mapema dakika ya tano kupitia kwa Zidane Sereri, aliyepokea pasi safi kutoka kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ndani ya eneo la hatari na kumalizia kwa ustadi dhidi ya kipa wa Dodoma Jiji, Daniel Mgore.

Dakika ya 12, Azam FC iliongeza bao la pili baada ya Feisal Salum kuitumia vizuri pasi kutoka kwa Sereri na kuiweka timu yake mbele kwa mabao 2-0 ndani ya dakika 15 za kwanza za mchezo.

Azam FC Yavunja Ukame wa Ushindi Ugenini Kwa Kuichapa Dodoma Jiji 3-0

Mabao hayo ya mapema yaliipa Azam FC udhibiti wa mchezo huku Dodoma Jiji, ambayo ilikosa huduma ya beki wake wa kati Abdi Banda kutokana na adhabu ya kufungiwa mechi tatu, ikijaribu kurejea kwenye mchezo.

Licha ya juhudi za wenyeji kujipanga upya, kipindi cha kwanza kilimalizika Azam FC ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili, kocha wa Dodoma Jiji Amaan Josiah alifanya mabadiliko dakika ya 59 kwa kumtoa Dickson Ambundo na kumuingiza Yassin Mgaza ili kuimarisha safu ya ushambuliaji akicheza sambamba na Faraji Kayanda.

Hata hivyo, Azam FC iliendelea kudhibiti mchezo na kuongeza bao la tatu dakika ya 71 kupitia tena kwa Zidane Sereri, baada ya walinzi wa Dodoma Jiji kujichanganya wakati wakijaribu kuokoa hatari iliyotokana na pasi ya chini ya Ashrafu Kibeku ndani ya boksi.

Bao hilo lilithibitisha ushindi wa Azam FC katika mchezo huo.

Sereri, aliyefunga mabao mawili katika mechi hiyo dhidi ya timu yake ya zamani ya Dodoma Jiji, alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi.

Kwa ushindi huo, Azam FC imepanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 27, sawa na Simba lakini ikitofautiana kwa wastani wa mabao.

Azam FC imefunga mabao 21 na kuruhusu manne, wakati Simba ikiwa imefunga mabao 20 na kuruhusu matano.

Matokeo hayo pia yanaipa Azam FC morali kuelekea mchezo wake ujao dhidi ya Yanga, utakaochezwa Machi 15, 2026 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Editor’s Picks:

  1. Ratiba ya 16 Bora Kombe la Shirikisho CRDB Federation Cup
  2. Mastaa Ligi Kuu Wavunja Rekodi Kombe la Shirikisho la CRDB Federation Cup
  3. Othmen Najjar Azungumzia Maandalizi ya Singida BS Kabla ya Kuivaa Yanga
  4. Azam vs Yanga Yaamishiwa Dimba la Chamazi
  5. Uwanja wa Mkapa Kufungwa Kupisha Maandalizi ya AFCON 2027
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo