Gamondi Apania Kumaliza Kazi Mapema Dhidi ya Vital’O
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameweka wazi azma yake ya kuhakikisha kikosi chake kinamaliza kazi mapema katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’O ya Burundi. Mtanange huo unatarajiwa kufanyika Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Gamondi, akizungumza baada ya mazoezi ya jana, alisisitiza umuhimu wa kutumia vyema kila nafasi itakayopatikana ili kupata ushindi wa kishindo utakaowapa ahueni kuelekea mchezo wa marudiano. “Tunataka twende kwenye mchezo wa marudiano tukiwa hatuna presha kubwa,” alisema Gamondi.
Katika mazoezi ya hivi karibuni, Gamondi amekuwa akiwasisitiza washambuliaji wake, akiwemo Jean Baleke, Prince Dube, Kennedy Musonda na Clement Mzize, kutumia nafasi zote zinazopatikana kufunga mabao bila kujali mpira uko upande gani wa uwanja.
Yanga imekuwa na safu kali ya ushambuliaji msimu huu, ikifunga mabao 13 na kuruhusu manne katika michezo sita iliyocheza hadi sasa. Katika michezo hiyo, wameshinda mitano na kupoteza mmoja.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kuwa wamejipanga vyema kwa mchezo huo wa kwanza na kuwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuwaombea dua ili washinde mabao mengi. “Tukishinda hivyo basi mechi ya marudiano ambayo kikanuni tutakuwa tunacheza nyumbani tunakwenda tu kumalizia malizia kazi, maana kwetu itakuwa kama mtoko tu,” alisema Kamwe.
Mechi ya Jumamosi itachezwa Uwanja wa Azam Complex, ambapo kikanuni Yanga itakuwa mgeni dhidi ya timu hiyo ya Burundi ambayo imeamua kuhamishia michezo yao hapa nchini. Baada ya mchezo huo, Yanga itarudia na Vital’O, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Agosti 24. Mshindi wa jumla kati ya timu hizo mbili atacheza na mshindi kati ya CBE ya Ethiopia au SC Villa ya Uganda katika hatua ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti