Majina ya Waliochaguliwa Kujiunga na Vyuo vya VETA 2026

Majina ya Waliochaguliwa Kujiunga na Vyuo vya VETA 2026

Jumla ya waombaji 14,433 wamechaguliwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa mwaka wa masomo 2026, kati ya waombaji 18,875 waliowasilisha maombi.

Miongoni mwa waliochaguliwa wamo pia wahitimu 134 wa elimu ya juu, wakiwemo wenye astashahada, shahada na shahada ya uzamili, hatua inayoonesha kuongezeka kwa uelewa wa umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mnamo Jumanne, Desemba 23, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, alisema mchakato wa uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia miongozo na mifumo rasmi ya Serikali, kwa lengo la kuhakikisha uwazi na usawa kwa waombaji wote.

“Jumla ya waombaji 14,433 wamepangiwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vya VETA kwa ngazi ya kwanza kwa mwaka wa masomo 2026. Kati yao wanaume ni 8,776 na wanawake ni 5,657,” alisema Kasore.

Majina ya Waliochaguliwa Kujiunga na Vyuo vya VETA 2026

Mgawanyo wa Masomo ya Asubuhi na Jioni VETA 2026

Kwa mujibu wa VETA, kati ya waliochaguliwa:

  • 12,942 watahudhuria masomo ya asubuhi
  • 1,491 wamepangiwa masomo ya jioni

Aidha, waombaji 4,511 bado wanasubiri kupangiwa vyuo na fani, hali inayotokana na kuchagua fani moja tu wakati wa maombi.

Kasore alibainisha kuwa fani ya umeme (Electrical Engineering) ilipokea idadi kubwa zaidi ya waombaji, huku fani ya ufundi mitambo (Mechanical Engineering) ikipata waombaji wachache ikilinganishwa na fani nyingine.

Walemavu na Usawa wa Elimu Vyuo vya VETA

Akizungumzia waombaji wenye mahitaji maalum, Kasore alisema jumla ya watu 195 wenye ulemavu waliomba kujiunga na mafunzo ya VETA kwa mwaka wa 2026.

“Kati ya waombaji wenye ulemavu, 145 wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na vyuo 53 vya VETA, huku 50 waliobaki wakiendelea kusubiri kupangiwa,” alisema, akiongeza kuwa wote watapata fursa ya kujiunga na mafunzo.

Alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila raia anapata fursa sawa ya elimu bila kujali hali ya kimwili, jinsia au kabila, kwa kuweka mazingira rafiki yanayowezesha kila mmoja kufikia ndoto zake.

Wahitimu wa Vyuo Vikuu Kujiunga na VETA 2026

Kuhusu wahitimu wa elimu ya juu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA alisema waombaji wenye shahada na shahada ya uzamili walioomba mafunzo ya ufundi stadi wamepangiwa vyuo, ingawa waombaji 11 bado wanasubiri kupangiwa fani na vyuo walivyochagua.

Hatua ya wahitimu wa vyuo vikuu kurejea VETA imeelezwa kuwa ni ishara ya mabadiliko chanya katika mifumo ya maandalizi ya vijana na mtazamo kuhusu mafunzo ya ufundi stadi.

Mkazi wa Makulu, Iddi Maalim, alisema mafunzo ya ufundi stadi yanatoa suluhisho la ajira kwa vijana kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo unaowawezesha kuanzisha biashara au kupata ajira kwa haraka. Alisisitiza kuwa si kila kijana anaweza kujiunga na chuo kikuu, hivyo VETA inakuwa mbadala muhimu.

Kwa upande wake, Asha Hassan alisema idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu kujiunga na VETA inaonesha umuhimu wa elimu ya ufundi stadi, na kuvunja dhana potofu kuwa mafunzo ya ufundi ni kwa wale wasio na elimu rasmi.

Jinsi ya Kupata MAJINA ya Waliochaguliwa Kujiunga na Vyuo vya VETA 2026

Kama wewe ni miongoni mwa maelfu ya waliotuma maombi ya kujiunga na kozi zinazotolewa katika vyuo vya VETA 2026 na unatafuta orodha ya waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetangaza rasmi majina ya waombaji waliofanikiwa kuchaguliwa kwa mwaka wa masomo 2026.

Majina ya waliochaguliwa yamechapishwa kupitia tovuti rasmi ya VETA, ambapo waombaji wanaweza kuyapitia kwa urahisi ili kuthibitisha kama wamepangiwa chuo na kozi husika. Orodha hiyo inajumuisha waombaji wa masomo ya asubuhi na jioni, pamoja na taarifa za waliopangiwa vyuo na wale wanaosubiri kupangiwa kutokana na kuchagua fani moja pekee.

Kupata majina ya waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vinavyomilikiwa na VETA kwa mwaka wa 2026 bonyeza viungo vilivyopo hapa chini

Bofya Hapa Kuona Majina

Bofya Hapa Kupakua Fomu za Kujiunga VETA

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba 2025/2026 NECTA
  2. Ratiba ya Mtihani wa Kidato cha Sita 2026
  3. Wanafunzi Waliochaguliwa Kidato Cha Kwanza 2026
  4. Form One Selection 2026 | Majina ya Waliochaguliwa Kidato cha Kwanza 2026
  5. Matokeo ya Kidato cha Nne 2024/2025 (NECTA Form Four Results)
  6. Botswana PSLE Results 2025 Released: 52,766 Candidates Sit Examination as Pass Rate Reaches 99.91%
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo