Timu Nane Zathibitishwa Kushiriki Kombe la Mapinduzi 2026 Zanzibar
Dar es Salaam. Timu nane zimethibitishwa kushiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026 yatakayofanyika Visiwani Zanzibar kuanzia mwishoni mwa Desemba 2025 hadi Januari 13, 2026, ikiwa ni kurejea kwa mfumo wa klabu baada ya msimu uliopita kushirikisha timu za taifa.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Desemba 28, 2025 na kufanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, huku baadhi ya kumbukumbu zikionyesha kuwa fainali ya msimu uliopita ilichezwa katika Uwanja wa Gombani, Pemba, ambapo Zanzibar Heroes ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Burkina Faso mabao 2-1.
Kwa mujibu wa ratiba na mpangilio wa mashindano hayo, Tanzania Bara itawakilishwa na klabu nne ambazo ni
- Yanga
- Simba
- Azam
- Singida Black Stars.
Upande wa Zanzibar utawakilishwa na klabu tatu ambazo ni Mlandege, KVZ na Fufuni, huku timu moja kutoka nje ya nchi ikiwa ni URA ya Uganda.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Machano Makame Haji, amesema uteuzi wa timu hizo umezingatia ushindani na historia ya mashindano hayo, akibainisha kuwa Mlandege ni bingwa wa Zanzibar kwa misimu ya 2023 na 2024. Ameongeza kuwa mashindano hayo yanalenga kuongeza ushindani wa kimataifa na kuimarisha hadhi ya soka la Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe, ametangaza ongezeko la zawadi kwa washindi wa Kombe la Mapinduzi 2026. Amesema bingwa wa kwanza atapata Shilingi milioni 150 pamoja na Kombe la Ushindi, huku mshindi wa pili akiondoka na Shilingi milioni 100.
“Mchezaji Bora wa Mechi katika hatua ya makundi atapata Shilingi milioni 1, katika robo fainali Shilingi milioni 2 na katika fainali Shilingi milioni 3,” amesema Pembe, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza hamasa na ushindani miongoni mwa wachezaji.
Machano Haji pia amewaomba mashabiki wa soka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi viwanjani kushuhudia mashindano hayo. “Nawaomba tusafiri pamoja katika jahazi hili ili tuweze kufikia malengo. Lengo kubwa ni kuhamasisha michezo katika nchi yetu ya Tanzania na hapa Zanzibar,” amesema.
Kombe la Mapinduzi limekuwa likifanyika kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 katika mfumo wa sasa, likiwa na lengo la kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Katika historia yake, klabu mbalimbali zimefanikiwa kutwaa ubingwa akiwemo Azam aliyebeba taji mara tano, Simba mara nne, Yanga mara mbili, pamoja na mabingwa wengine kama URA, KCCA, Mtibwa Sugar, Miembeni, Mlandege na Zanzibar Heroes.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba Ya AFCON 2025 Hatua Ya Makundi
- Kikosi cha Taifa Stars AFCON 2025
- Matokeo ya Coastal Union vs Yanga Leo 07/12/2025
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
- Ratiba ya Mechi za Leo 07/12/2025 Ligi Kuu ya NBC
- Makundi ya Kombe la Dunia 2026
- TFF Yatangaza Kikosi cha Awali cha Taifa Stars kwaajili ya Fainali za AFCON 2025 Morocco









Leave a Reply