Timu Zilizopanda Daraja Ligi Kuu Tanzania 2025/2026
Msimu wa 2024/2025 wa Ligi ya Daraja la Kwanza Tanzania (Championship) unaelekea ukingoni, huku baadhi ya vilabu vikubwa vikiwa tayari vimejihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, inayojulikana kama NBC Premier League, kwa msimu wa 2025/2026. Vilabu hivi vimeonyesha kiwango cha juu cha ushindani, ustahimilivu na nidhamu ambayo imewasaidia kurejea kwenye ngazi ya juu ya soka nchini. Kwa msimu ujao, mashabiki wanatarajia kuona ushindani mkali kutoka kwa timu hizi ambazo zimepanda daraja kwa njia ya kuvutia.
1. Mbeya City: Urejeo wa Kishindo NBC Premier League
Klabu ya Mbeya City kutoka mkoani Mbeya imerejea rasmi katika Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2025/2026 baada ya kushuka daraja msimu wa 2022/2023. Katika msimu huu wa Championship 2024/2025, Mbeya City imeonesha kiwango cha juu cha ushindani, na hatimaye kufanikisha kurejea kwa kishindo kupitia ushindi mkubwa wa mabao 5-0 dhidi ya Cosmopolitan.
Ushindi huo muhimu, uliopatikana katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, uliiwezesha timu hiyo kufikisha pointi 65 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yeyote kutoka nafasi ya tatu kushuka chini. Mabao ya ushindi huo yalifungwa na Riphat Khamis (mabao mawili), Eliud Ambokile, Faraji Kilaza Mazoea na David Mwasa.
Mbeya City, ambayo ilicheza Ligi Kuu kwa misimu kumi mfululizo tangu ilipopanda kwa mara ya kwanza mwaka 2013/2014, ilishuka daraja mwaka 2023 baada ya kushindwa mechi za mchujo dhidi ya KMC na Mashujaa. Kurejea kwao kunapokelewa kwa furaha na mashabiki wa soka mkoani Mbeya ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu timu yao kurejea katika ligi kuu.
2. Mtibwa Sugar: Kurejea kwa Timu ya Kihistoria
Mtibwa Sugar, klabu maarufu yenye maskani yake Manungu, Turiani, Morogoro, nayo imerejea rasmi katika Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2025/2026. Timu hii ilishuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2023/2024, lakini ikajipanga upya kwa mafanikio makubwa katika msimu huu wa NBC Championship.
Hadi kufikia hatua ya kupanda daraja, Mtibwa Sugar ilikusanya jumla ya alama 67 katika mechi 28, na kuwa kinara wa ligi hiyo. Timu hii ilionesha uwezo mkubwa licha ya changamoto walizokutana nazo, ikiwa ni pamoja na kupoteza baadhi ya mechi dhidi ya Geita Gold na Kiluvya FC. Mojawapo ya mechi muhimu zilizochangia mafanikio yao ilikuwa dhidi ya Mbeya City ambapo Mtibwa Sugar walishinda kwa mabao 3-1. Ushindi huu uliimarisha nafasi yao ya kurejea Ligi Kuu.
Kurejea kwa Mtibwa Sugar ni habari njema kwa wapenzi wa soka, hasa wa mkoa wa Morogoro, kutokana na mchango mkubwa wa klabu hiyo katika kukuza vipaji vya soka nchini. Pia, ni matarajio ya wengi kuwa timu hii ya kihistoria itaongeza ushindani wa kweli katika msimu ujao wa ligi kuu dhidi ya vilabu vikubwa kama Simba SC, Young Africans na Azam FC.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ambokile Aitega Mbeya City Baada Ya Kupanda Daraja
- Napoli Yabeba Kombe la Serie A kwa Mara ya Nne Baada Vita Kali Dhidi ya Inter
- Fiston Mayele Awaumiza Vichwa Mamelodi Kuelekea Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika
- Viingilio Mechi ya Marudiano Simba Vs RS Berkane 25/05/2025
- Muonekano wa Kombe Jipya La Klabu Bingwa CAF Champions League
- Dk. Mwinyi Ailipa Simba Ada ya Uwanja Fainali Kombe la Shirikisho!
- Kikosi cha RS Berkane Chatua Tanzania Kikiwa na Presha ya Simba Jumapili
Leave a Reply