Wasafi Festival 2024: Diamond Aanzisha Drama Nyingine

Wasafi Festival 2024: Diamond Aanzisha Drama Nyingine

Tamasha la Wasafi Festival 2024 limezinduliwa kwa kishindo, lakini sio bila drama. Msanii mkubwa Diamond Platnumz ameibua gumzo tena kuhusu uhusiano wake na baba yake, Mzee Abdul.

“Nimelelewa na Mama Tu”

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Diamond alimshukuru mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ almaarufu Mama Dangote, kwa kumlea na kumfanya awe alivyo leo. Alisema wazi kuwa hakulelewa na baba, na hii sio mara ya kwanza kusema hivyo hadharani.

Kauli hii imezua hisia kali miongoni mwa mashabiki na waangalizi wa muziki, haswa ikizingatiwa historia ya Diamond na Mzee Abdul.

Pia katika hotuba yake, Diamond alimshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika sanaa, huku akimtaja kuwa mfano bora wa uongozi wa mwanamke nchini.

Diamond alisema kwamba, kwa sababu alilelewa na mama yake pekee, anaamini katika uwezo wa wanawake, akimtaja mama yake kama mfano wa kuigwa kutokana na juhudi zake za kumlea na kumfikisha kwenye mafanikio yake ya sasa.

“Nawashukuru sana wanawake wapambanaji. Mimi nililelewa na mama yangu pekee, na ni yeye ambaye alihangaika nami hadi leo nimefika hapa. Ninaamini wanawake wana uwezo wa kufanya makubwa kama ilivyo kwa Mama Dangote na Rais Samia,” alisema Diamond

Wasafi Festival 2024: Diamond Aanzisha Drama Nyingine

Ahadi za Diamond Kwa Mashabiki

Mbali na mijadala ya kifamilia, Diamond aliitumia fursa hiyo pia kuwapa mashabiki wake taarifa kuhusu mipango yake ya siku za usoni. Alibainisha kuwa Wasafi Festival 2024 itaanzia Ruangwa, Mkoa wa Lindi, na akaahidi kuendelea kuleta burudani ya kipekee kwa wapenzi wa muziki wa Bongo Flava. Pia, alitangaza mpango wake wa kuzindua bidhaa mpya, hatua inayodhihirisha azma yake ya kuwa miongoni mwa wafanyabiashara tajiri duniani.

“Nina ndoto ya kuwa tajiri namba moja duniani, na mwaka huu natarajia kutambulisha bidhaa yangu mpya. Naomba muendelee kunishika mkono ili tufikie mafanikio hayo pamoja,” alisema Diamond.

Historia ya Mgogoro na Baba Mzazi

Drama ya kifamilia inayomzunguka Diamond si mpya. Mwaka 2022, Diamond aliweka wazi kwamba Mzee Abdul si baba yake mzazi, bali baba yake halisi alikuwa mzee Nyange, ambaye kwa sasa ni marehemu. Taarifa hii ilileta taharuki mitandaoni na kuibua mjadala mzito kuhusu uhusiano wa Diamond na Mzee Abdul, ambaye alimlea msanii huyo tangu utoto.

Kwa mujibu wa mahojiano aliyoyafanya na Wasafi Radio, Diamond alisema kwamba alipokuwa na umri wa miaka 11, alifahamishwa na jirani yake kuhusu baba yake halisi, jambo lililomshangaza kutokana na utofauti aliokuwa akiuhisi katika malezi yake. Hali hiyo ilisababisha gumzo kubwa baada ya Mama Dangote kuweka wazi kuwa Mzee Abdul hakuwahi kuwa baba wa kumzaa Diamond, bali alikuwa mlezi.

Mzee Abdul Abwaga Moyo Chini

Baada ya miaka kadhaa ya mijadala kuhusu uhalali wa kuwa baba wa Diamond, Mzee Abdul alionekana kukubali hali hiyo na kusitisha mjadala huo. Katika mahojiano ya hivi karibuni, Mzee Abdul alisema kuwa amelipokea suala hilo kwa moyo mmoja na kumwachia Mungu.

“Nilishamuachia Mungu suala hili. Kama anasema amelelewa na mama yake pekee, basi sawa. Mimi nimeamua kukaa pembeni,” alisema kwa huzuni Mzee Abdul, akiashiria kukubali hali hiyo baada ya miaka mingi ya sintofahamu.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Wasanii Wanaowania Tuzo za Muziki Tanzania TMA 2023/2024
  2. Mahakama yamtaka Harmonize kuilipa CRDB Sh113 milioni
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo