Yanga Sc Mbioni Kubeba Ubingwa Wa Ligi Kuu Ya NBC 2023/2024: Young Africans (Yanga) imeongeza matumaini yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 baada ya kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika jana May 5. Joseph Guede alifunga bao pekee la Yanga katika dakika ya 41 akimalizia pasi safi kutoka kwa Mudathir Yahya.
Yanga Sc Mbioni Kubeba Ubingwa Wa Ligi Kuu Ya NBC 2023/2024
Guede amefunga jumla ya mabao matano tangu ajiunge na Yanga katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo. Ushindi huu umewafanya vinara hao wa Jangwani kufikisha pointi 65 baada ya kucheza mechi 25, wakizidi kuimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya NBC Tanzania.
Wababe hao wa Ziwa Tanganyika watalazimika kupambana kiume katika mechi zao zilizosalia ili kuepuka kushuka daraja baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Yanga Sc. Mashujaa FC wana pointi 23 kutoka mechi 25 na kwasasa wapo nafasi ya 14. Iwapo timu hiyo itashinda mechi zake zote tano zilizosalia, kinadharia wanaweza kufikisha pointi 38.
Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga, alikiri kuwa mchezo ulikuwa mgumu na kuwapongeza vijana wake kwa kupata ushindi huo.
“Ilikuwa mechi ya ushindani, Mashujaa FC walileta changamoto japo hawakuwa na shuti lililolenga lango. Hata hivyo, tulikuwa na dhamira ya kupata pointi tatu, na tumefanikiwa. Sasa tunaelekeza nguvu kwenye mechi zilizosalia,” alisema Gamondi.
Mechi inayofuata ya Yanga itakuwa dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, tarehe 8 Mei saa 1 usiku, kisha wataifuata Mtibwa Sugar ugenini tarehe 13 Mei, saa 10 jioni, halafu Dodoma Jiji FC kwenye Uwanja wa Jamhuri, tarehe 22 Mei saa 10 jioni.
Mechi zingine zinazowasubiri Yanga ni dhidi ya Tabora United tarehe 25 Mei kwenye uwanja wa Azam Complex, na kufuatiwa na Tanzania Prisons tarehe 28 Mei.
Wakati huo huo, vinara wengine, Simba na Azam FC, watakumbana na wapinzani wagumu, Mtibwa Sugar na Tabora United katika muendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye viwanja vinne.
Azam FC watasafiri hadi kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani mkoani Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar saa kumi jioni, wakati Simba watawakaribisha Tabora United kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam saa 12:15 jioni.
Mechi zingine ni Ihefu FC dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Liti, mkoani Singida na Coastal Union dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani saa 2:30 usiku.
Mechi hizi ni muhimu kwa timu zote nane kuboresha nafasi zao kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Azam FC wanalenga kupata ushindi ili kuendelea kuisukuma Yanga wanaongoza ligi.
Wamejipanga kuwazidi watani wao Simba ambao wana pointi 50 kutoka mechi 24.
Mtibwa Sugar nao wanapambania ushindi dhidi ya Azam FC ili kuepuka kushuka daraja kwani kwasasa wapo mkiani na pointi 17 kutoka mechi 24.
Weka Komenti