NMB Yaungana na Yanga Kuelekea Ligi ya Mabingwa Afrika
Katika maandalizi ya kuelekea mtanange wa marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CBE SA ya Ethiopia, Mabingwa watetezi wa Ligui kuu ya NBC Tanzania Yanga wamepata nguvu mpya baada ya Benki ya NMB kutambulishwa rasmi kama mmoja wa wadhamini wa mechi hiyo muhimu katika kufuzu makundi ya klabu bingwa. Ushirikiano huu, uliobeba kauli mbiu ya “Timu Bora, Benki Bora,” unalenga kuimarisha safu ya mafanikio ya Yanga katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Yanga SC itashuka dimbani Jumamosi, Juni 21, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ikiwa na lengo la kulinda ushindi wao wa bao 1-0 walilolipata katika mechi ya awali jijini Addis Ababa. Mshindi wa jumla atafuzu kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua muhimu kwa klabu hiyo kuimarisha jina lake katika soka la kimataifa.
Kwa mujibu wa Meneja Biashara wa NMB Zanzibar, Bi. Naima Said Shaame, uamuzi wa benki hiyo kuidhamini Yanga unatokana na mafanikio makubwa ya klabu hiyo, yanayoakisi ushindi wa kitaifa na kimataifa. “Tumeona umuhimu wa kuipa nguvu Yanga kutokana na mafanikio yao. NMB inaamini katika kuunga mkono timu yenye mafanikio kama Yanga ambayo tayari imeshinda Ngao ya Jamii na kufuzu raundi hii kwa kuwashinda Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0,” alisema Bi. Naima.
Ushirikiano wa Kipekee kati ya NMB na Yanga
NMB imeonyesha dhamira thabiti ya kuendelea kushirikiana na Yanga, si tu katika mchezo huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, bali pia katika miradi mingine muhimu inayowahusisha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo. Benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kurahisisha usajili wa wanachama wa Yanga kupitia kadi maalum zinazopatikana kwenye matawi ya NMB kote nchini.
Bi. Naima aliwahimiza mashabiki wa Yanga kutumia fursa hiyo kurasimisha ushabiki wao kwa kujiunga rasmi na uanachama wa klabu yao kupitia huduma za NMB. “Tunawahimiza mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kujiunga na uanachama rasmi. Hii itasaidia kuongeza nguvu kwa timu yao wanayoipenda na kuongeza mapato muhimu kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya klabu,” aliongeza.
Ushindi Wanaoutarajia Yanga
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, aliwapongeza NMB na wadhamini wengine wote walioungana na klabu hiyo kwa lengo la kuiunga mkono kuelekea hatua za kimataifa. “Tunawashukuru NMB kwa kuonyesha nia ya dhati ya kushirikiana nasi.
Ushirikiano huu unaleta motisha zaidi kwa wachezaji na mashabiki wetu kuelekea kufuzu kwa mara ya tatu katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Arafat.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka klabu ya Yanga, kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 200 tayari kimeingizwa kwenye akaunti ya klabu hiyo kabla hata ya kuanza kwa mauzo rasmi ya tiketi za mechi, kutokana na udhamini kutoka NMB na wadau wengine.
Ratiba ya Matukio ya Yanga Kabla ya Mechi
Ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea mechi dhidi ya CBE, klabu ya Yanga imeandaa ratiba maalum itakayoanza kwa dua maalum siku ya Ijumaa kwenye Madrassat Swifatul Nnabawwiyah, Zanzibar. Baada ya swala ya Ijumaa, viongozi wa klabu hiyo watatoa misaada kwa watoto yatima, hatua inayoonesha kujali jamii inayowazunguka.
Pia, Yanga imeleta kikosi chake kamili Zanzibar isipokuwa Farid Mussa Maliki ambaye ni majeruhi. Kocha wa Yanga amesisitiza kuwa, kikosi hicho hakina muda wa kupoteza kwani ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara ni ngumu, hivyo wachezaji wote wanahitajika kuendelea kuwa pamoja katika maandalizi ya michezo inayofuata.
Wadhamini Wengine Wanaoiunga Mkono Yanga
Mbali na NMB, wadhamini wengine walioungana na Yanga kwa ajili ya mechi dhidi ya CBE ni pamoja na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirika la Bima Zanzibar, Inuka Fund, PBZ, na ZIPA. Wote hawa wanajiunga na wadhamini wa kudumu wa klabu hiyo kama GSM, SportPesa, na Azam TV, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Yanga.
Kwa ushirikiano huu, Yanga inatarajia kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuendelea kudhihirisha ukubwa wake kwenye soka la Afrika.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Gamondi Aweka Wazi Nia Yake ya Kutwaa Ubingwa wa Afrika
- Barcelona Yaanza UEFA Kwa Kichapo cha 2-1 Kutoka kwa Monaco
- Manchester City washindwa kutamba dhidi ya Inter
- Arsenal Yaambulia Pointi Moja Ugenini, Raya Aokoa Mkwaju wa Penalti
- Msimamo NBC Premier league 2024/2025 | Ligi Kuu Bara
- Gadiel Aanza Kazi Chippa United, Majogoro Kicheko
- Azam FC Yaichapa KMC 4-0, Taoussi Aanza Kugawa Dozi
Weka Komenti