Kengold Wakijichanganya Tunawapiga Nyingi, Gamondi Atoa Onyo
Katika kuelekea mchezo kati ya Yanga SC na Ken Gold, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ametoa onyo kali kwa wapinzani wake akisisitiza kuwa lengo lake kuu ni kuondoka na pointi tatu, lakini akiongeza kuwa, endapo wapinzani wao wakifanya makosa, basi watafungwa mabao mengi.
Yanga SC imekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, hasa katika safu ya ushambuliaji.
Katika mechi tano zilizopita, Yanga imeshinda kwa jumla ya mabao 19, ikiwa ni pamoja na ushindi wa mabao sita katika mchezo wa mwisho dhidi ya CBE kwenye hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika. Wakiwa na msukumo wa ushindi huo, Yanga wanajitayarisha kuwakabili Ken Gold ambao hawana pointi hata moja baada ya kupoteza michezo minne mfululizo kwenye Ligi Kuu.
Gamondi: “Tunataka Pointi Tatu, Lakini Wakijichanganya Tunawapiga Nyingi”
Akizungumza jijini Dar es Salaam, kocha Gamondi alieleza kuwa kipaumbele chake ni kushinda na kupata pointi tatu, bila kujali idadi ya mabao watakayofunga. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kama timu yake itapata nafasi ya kufunga mabao mengi zaidi, wataitumia ipasavyo.
“Mimi kiu yangu ni Yanga kupata pointi tatu hata kwa bao moja ni sawa, ila kama tutapata nafasi ya kufunga zaidi tutafanya hivyo na itakuwa nzuri zaidi, nimewaandaa vyema wachezaji wangu, alisema Gamondi.”
Licha ya wapinzani wao kuwa kwenye hali mbaya, Gamondi alisema kuwa hawawadharau Ken Gold kwani ni timu mpya iliyopanda Ligi Kuu, na kwa hiyo wana haki ya kucheza kwenye ligi hiyo kwa uwezo wao. Alisisitiza kuwa, mbinu walizozitumia dhidi ya wapinzani wengine zitaendelea kutumika, akiamini kuwa maandalizi yao ni thabiti.
Kikosi Cha Yanga Kiko Tayari Licha ya Uwepo wa Majeruhi
Katika maandalizi ya mchezo huo, Gamondi alifafanua kuwa wachezaji wote wamesafiri na wako fiti, isipokuwa Farid Mussa ambaye anasumbuliwa na majeraha. Hata hivyo, kocha huyo alieleza kuwa Yanga inao wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu na anajivunia kina chake kikosi, jambo linalompa uhuru wa kubadilisha kikosi kulingana na mahitaji ya kila mechi.
“Ni juzi tumecheza mechi ya klabu bingwa na kesho tuko uwanjani, sina hofu yoyote na badala yake nitaangalia nani aanze au kusubiri kutokana na upana wa kikosi changu binafsi nafurahia ratiba, aliongeza Gamondi.”
Kwa upande wa ratiba ngumu ambayo Yanga inakutana nayo, Gamondi alisema kuwa hana wasiwasi na uchovu wa wachezaji wake kwani wengi wao wana uzoefu wa kucheza mechi nyingi na wameandaliwa kushinda chini ya hali yoyote.
Aziz Andambwile: “Tunaijua Historia, Hatutawadharau Ken Gold”
Mchezaji mahiri wa Yanga, Aziz Andambwile, naye aliongeza kauli ya tahadhari akieleza kuwa, licha ya ubora wa Yanga kwa sasa, hawawezi kuwadharau Ken Gold. Alisisitiza kuwa wachezaji wa Yanga wamejifunza kutokana na historia, hasa baada ya kupoteza mara kadhaa kwenye michezo ya awali mkoani Mbeya dhidi ya Ihefu.
“Lazima tuwaheshimu wapinzani kwakuwa historia tunaikumbuka, tutacheza kwa umakini kulingana na kocha alivyotuelekeza kuhakikisha pointi tatu tunaondoka nazo na kujiweka pazuri, alisema Andambwile.”
Aziz alifafanua kuwa wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huu kwani ushindi utaweka Yanga kwenye nafasi nzuri zaidi katika mbio za ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Azam FC Kwenye Mtihani Mzito Zanzibar Dhidi ya Simba
- Takwimu za Chama Yanga zaanza kutisha Klabu Bingwa
- Hizi Ndio Timu 5 Ambazo Bado Hazijashinda Mechi yoyote Ligi Kuu
- Aziz KI Afichua Kilichomo Kwenye Mkataba Wake na Yanga
- Ratiba ya Mechi ya Leo 25 September 2024
- Kengold Vs Yanga Leo 25/09/2024 Saa Ngapi
- Timu Zilizofuzu Makundi CAF 2024/2025
- Timu zilizofuzu Makundi Kombe La Shirikisho CAF 2024/2025
Weka Komenti