Tabora United Yashindwa Kutamba Nyumbani
Tabora United imeshindwa kuendeleza ushindi mbele ya mashabiki wake baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora. Hii ilikuwa mechi ya nne ya Tabora United katika msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/2025, ambapo walitarajiwa kuonesha ubora wao baada ya ushindi mfululizo dhidi ya Namungo FC na Kagera Sugar.
Tabora United, timu iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita kupitia mechi za mtoano dhidi ya Biashara United, ilianza msimu kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba SC. Hata hivyo, walizinduka haraka na kushinda michezo miwili mfululizo dhidi ya Namungo FC na Kagera Sugar, jambo lililowapa matumaini mashabiki wao wa nyumbani.
Walipowakaribisha Tanzania Prisons, walitarajiwa kuendeleza ubabe wao na kuongeza pointi zaidi, lakini hali haikuwa kama walivyotarajia.
Licha ya matumaini ya ushindi wa nyumbani, Tabora United walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Prisons ambao, hadi sasa, hawajafanikiwa kupata ushindi wowote msimu huu.
Prisons, timu inayojulikana kwa ulinzi wake thabiti, walifanikiwa kuzuia mashambulizi ya Tabora na kuwalazimisha kutoka sare ya tatu mfululizo. Prisons walitoka sare ya 0-0 na Pamba Jiji pamoja na Mashujaa katika michezo yao iliyotangulia.
Nyota wa mchezo alikuwa beki wa kati wa Tabora United, Kelvin Pemba, ambaye alicheza kwa kiwango cha juu dhidi ya mshambuliaji hatari wa Prisons, Samson Mbangula. Mashabiki waliokuwepo walionekana kufurahia sana jinsi Pemba alivyomzuia Mbangula, na kumshangilia mara kwa mara kwa uchezaji wake bora.
Kosa Kosa za Nafasi za Mabao kwa Tabora
Licha ya nafasi kadhaa walizotengeneza, washambuliaji wa Tabora United walishindwa kutumia fursa hizo kuipatia timu yao ushindi. Mchezaji Yacouba Songne alipoteza nafasi muhimu ambazo zingeweza kubadilisha matokeo ya mchezo huo. Mchezaji mwingine muhimu kwa Tabora, Salum Chuku, aliumia na kulazimika kuondolewa uwanjani kwa gari la wagonjwa, na baadaye kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete kwa matibabu. Kwa mujibu wa taarifa za daktari wa timu, Chuku alitarajiwa kurejea kikosini baada ya hali yake kutengemaa.
Maoni ya Makocha Baada ya Mchezo
Baada ya mchezo huo, kocha wa Tanzania Prisons, Mbwana Makatta, alisema kuwa sare hiyo ni mafanikio kwa timu yake kwa sababu bado hawajaruhusu kufungwa katika mechi zote za ugenini. “Wachezaji wetu wameonesha uwezo mkubwa uwanjani.
Ingawa hatukufanikiwa kufunga, tulijitahidi kumaliza mchezo kwa sare. Tulicheza kwa nidhamu kubwa, hasa kipindi cha pili, na kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hatukuzitumia vizuri,” alisema Makatta.
Kwa upande wake, kocha wa Tabora United, Francis Kimanzi, alitaja uchovu wa wachezaji wake kutokana na kucheza mechi tatu ndani ya siku chache kama sababu ya kutopata ushindi. “Timu yetu haikupata muda wa kutosha kupumzika baada ya mchezo wetu uliopita.
Hata hivyo, najivunia juhudi za wachezaji wangu ambao walipambana sana. Tunajipanga kwa mechi ijayo dhidi ya Fountain Gate ili kupata matokeo bora zaidi,” alisema Kimanzi.
Nafasi ya Tabora United Katika Msimamo wa Ligi
Matokeo hayo yameiweka Tabora United katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, wakiwa na pointi saba, sawa na Mashujaa FC, lakini wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Vinara wa ligi kwa sasa ni Singida Black Stars, wenye pointi tisa baada ya mechi tatu. Kwa upande wa Tanzania Prisons, sare hiyo imewaongezea alama moja na kufikisha pointi tatu kutokana na michezo mitatu ya mwanzo ya msimu
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti