Timu za Tanzania Zilizofuzu Klabu Bingwa Afrika 2024/2025 | Wawakilishi wa Tanzania CAF Champions league
Michuano ya klabu bingwa Afrika 2023/2024 imeshuhudia tamati ya kusisimua, huku klabu kongwe za Tanzania, Yanga SC na Simba SC, zikionyesha tena ubabe wao. Baada ya msimu wa kihistoria ambapo Tanzania ilijivunia kuwa nchi pekee Afrika Mashariki na Kati kuwa na wawakilishi wawili kwenye robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika, mashabiki wa soka nchini wameingiwa na hamu kubwa kujua kama miamba hii miwili itaweza kurudia au hata kuvuka mafanikio hayo msimu ujao.
Msimu wa 2023/2024 utabaki kwenye kumbukumbu za mashabiki wa soka Tanzania kama moja ya misimu bora kwa vilabu vya nchi hii. Licha ya Yanga SC na Simba SC kutolewa kwenye robo fainali, timu zote zilionyesha kiwango cha juu cha soka, na kuvutia hisia za mashabiki kote Afrika. Yanga SC, licha ya kuondolewa na Mamelodi Sundowns kwa mikwaju ya penalti, walipambana vilivyo na kuonyesha soka la kuvutia. Tukio la kukumbukwa ni mkwaju wa Stephane Aziz Ki ambao ulionekana kuvuka mstari wa goli, lakini uamuzi wa mwamuzi ulionekana kuwa na utata, na hivyo kupelekea mechi kuamuliwa kwa penalti.
Simba SC, kwa upande wao, walikumbana na kibarua kigumu dhidi ya Al Ahly, wakifungwa katika mechi zote mbili. Hata hivyo, walipambana kwa ari na kujituma, wakionyesha uwezo wao dhidi ya moja ya timu bora barani Afrika. Licha ya kuondolewa mapema, misimu huu umeacha alama kubwa kwa soka la Tanzania. Wachezaji wengi wa Kitanzania wamepata kutambulika kimataifa, na vilabu vya Tanzania vimepata kuheshimika zaidi. Hii ni ishara kuwa soka la Tanzania linaendelea kukua na kuwa na ushindani mkubwa zaidi kimataifa.
Timu za Tanzania Zilizofuzu Klabu Bingwa Afrika 2024/2025
Wawakilishi wa Tanzania CAF Champions league msimu wa 2024/2025 ni Yanga Sc na Azam Fc.
Yanga SC, mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya NBC, wamejihakikishia nafasi kwenye Klabu Bingwa Afrika 2024/2025 kwa kishindo, wakimaliza msimu kwa kuvuna pointi 80 katika mechi 30. Ubingwa huu unaashiria uthabiti na ubora wa Wananchi, ambao sasa wanaweka macho yao kwenye ushindi wa kimataifa.
Azam FC, kwa upande wao, wamepata tiketi yao ya Klabu Bingwa Afrika kwa kumaliza katika nafasi ya pili ya ligi kuu, wakikusanya pointi 69 – idadi sawa na Simba SC walioshika nafasi ya tatu. Azam FC ilijihakikishia nafasi ya pili kwa kuwa na utofauti bora wa magoli (+42) ikilinganishwa na Simba SC (+34). Mafanikio haya ya Azam FC yanaonyesha ukuaji wao wa kasi katika soka la Tanzania, na sasa wanapata fursa ya kujipima dhidi ya vigogo vya Afrika.
Mapendekezo Ya Mhariri:
- Timu Zilizofuzu Klabu Bingwa Afrika 2024/2025
- Muonekano wa Kombe La CRDB Federation Cup 2023/2024
- Harry Kane Ndio Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu Ulaya 2023-2024
- Timu Inayoongoza kwa Magoli Ligi Kuu Ya NBC 2023/2024
- Timu zilizopanda Daraja Ligi Kuu ya England EPL 2024/2025
- Picha Za Parade ya Yanga SC Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2023/24
- Matokeo na Ratiba ya Kufuzu Kombe la Dunia 2026
Weka Komenti