Azam yaifuata Yanga Nusu Fainali Kombe La Shirikisho 2024
Mabingwa watetezi wa Kombe la FA Tanzania, Yanga kutoka Dar es Salaam, wameanza maandalizi yao kwa mechi ya nusu fainali dhidi ya Ihefu itakayochezwa Mei 19 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Nusu fainali nyingine itawakutanisha Azam FC na Coastal Union Mei 18 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ratiba rasmi ya michuano imetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufuatia kukamilika kwa mechi za robo fainali. Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Namungo katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Kipre Junior alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 10 ambapo Idd Seleman ‘Nado’ na Feisal Salum ‘Fei Toto’ walifuatia. Ayoub Semtawa alirudisha goli moja kwa Namungo kabla ya mapumziko. Gibril Sillah alifunga bao la ushindi kwa Azam FC dakika ya 52.
Pamoja na ushindi huo, Kocha Mkuu wa Azam Yousuopha Dabo, alikiri ugumu wa mechi. Aliisifia timu yake kwa kuanza vizuri lakini pia akasisitiza umuhimu wa kudumisha kasi kwa mchezo mzima.
Msemaji wa TFF, Clifford Ndimbo, amethibitisha kuwa mechi zote za nusu fainali zitaanza kuchezwa majira ya saa 9:30 mchana.
Ihefu ilifuzu kwa kuishinda Mashujaa FC kwa mikwaju ya penati baada ya sare ya 0-0, huku Coastal Union ikishinda dhidi ya Geita Gold kwa bao 1-0.
Yanga ilijihakikishia nafasi katika nusu fainali baada ya kuitandika Tabora United mabao 3-0.
Fainali ya Kombe la shirikisho mwaka huu itafanyika Uwanja wa Tanzanite, Babati, Mkoa wa Manyara.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti